Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limeamshikilia Askari No. F 4965 PC
Joel Francis almaarufu Masai kwa tuhuma za kumpiga na kumsabibishia kifo
kijana Donald Magalata ambaye alikuwa akiishi naye kama ndugu.
Tukio hilo lilitokea Januari mosi mwaka huu majira ya saa 7 usiku katika kambi ya polisi Mabatini jijini Mwanza.
Askari huyo anadaiwa kufanya tukio hilo mara baada ya kubaini kuwa
katika pochi yake iliyokuwa na kadi mbili za benki na kitambulisho cha
kazi havipo hali iliyosababisha mzozo baina yake na kijana huyo na
hivyo kulazimika kumuadhibu.
Tukio hilo lilotia simanzi kubwa kwa baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza ambao walifanikiwa kulishuhudia tukio hilo.
Mnamo Januari mosi majira ya usiku askari Joel Francis baada ya
kutoka kazini alifika nyumbani kwake na kumkuta Kijana Donald Magalata
akiwa amelala ndani kwake kwani alikuwa akimsaidia askari huyo kazi za
nyumbani.
Baada ya mtuhumiwa huyo kubaini kupoteza vitu vyake alilazimika
kumuuliza kijana huyo ambaye alidai kutokuviona jambo lililosabisha
mvutano kati yao.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza Justus Kamugisha amesema kuwa
mtuhumiwa alimpiga kijana huyo ndipo alipopiga kelele kuomba msaada na
mara baada ya kuokolewa alikimbizwa hospital lakini aliweza kupoteza
maisha na amesema mtuhumiwa yupo mahabusu akiendelea kufanyiwa
mahojiano.
Wengi katika mtaa huu wamebaki na mshangao wakiwa hawaamini kile
wanachokiona kwa askari huyo kuweza kufanya kitenda cha kinyama kwa
binadamu mwenzake.
Majira ya asubuhi Mwili wa Marehemu Donald Umefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
