Na Emmanuel Senny, Kigoma
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameiagiza
Mamlaka ya Bandari mkoani Kigoma (TPA) kupitia upya zoezi
linalolalamikiwa na wananchi kuhusu fidia.
Akizungumza
na wananchi baada ya kufungua soko jipya la Samaki lililoko kata ya
Kibirizi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, Waziri Majaliwa alisema kuwa,
katika kutekeleza miradi ya maendeleo kuna wananchi walioathirika baada
ya kutakiwa kupisha miradi hiyo.
Alisema
kuwa, kisheria wananchi wote wanaohamishwa katika maeneo yao hutakiwa
kulipwa fidia ambapo katika mradi wa upanuzi wa bandari ya Kigoma ambao
ulipeleka kuhamishwa kwa baadhi ya wananchi wa Kibirizi, wapo waliolipwa
fidia na wengine hawakulipwa huku wengine wakilalamikia kulipwa fidia
ndogo.
“Nimeona
wananchi wakiwa na mabango wakinihitaji niwasaidie katika suala la
fidia na wanadai haki haikutendeka pia hata Mbunge wao Zitto Kabwe
amegusia malalamiko ya wananchi ” alisema Waziri Majaliwa.
Aidha
Majaliwa alisema kuwa, Mamlaka ya bandari inatakiwa kupitia upya suala
la fidia kwa wananchi wa kibirizi kwa kukagua kila eneo la mtu na
thamani ya pesa aliyolipwa pia kuwalipa wale ambao hawakulipwa.
“Suala
la hili litafanyika mara moja mara baada ya mimi kuonana na viongozi wa
mamlaka ya bandari na nitahitaji kama kuna mtu alilipwa fidia ndogo
basi aongezwe kulingana na thamani ya eneo lake na kwa wale ambao
hawajalipwa kama maeneo yao yako kwenye mradi basi walipwe mara moja ”
alisisitiza Waziri Majaliwa.
Hata
hivyo Waziri Majaliwa alisema kuwa, suala la utekelezaji wa miradi ya
maendeleo ni endeleavu ambapo kwa Kigoma kuna mradi wa upanuzi wa
bandari na ujenzi wa bandari ya nchi kavu na miradi hii yote inagusa
maeneo ya wananchi hivyo serikali inatakiwa kulipa fidia stahiki kwa
kila mwananchi wa eneo husika.
Awali
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Majaliwa
kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu suala la fidia ambalo
linaonekana kuwa kero kutokana na wengi kulipwa fidia ndogo huku wengine
kutokulipwa kabisa.
“Kama
unavyoona Mheshimiwa Waziri Mkuu mabango ya wananchi wanaomba uwasaidie
katika suala hili maana kama miradi hii ni kwa lengo la kuleta
maendeleo basi wananchi waiunge mkono ila hawawezi kuunga mkono kama
mamlaka husika haziwalipi fidia zao kama kama thamani ya maeneo yao
ilivyo ” alisema Kabwe.