Rais Magufuli ampa maagizo mazito Waziri wa mambo ya nje

Wakati wakimbizi kutoka Burundi wakiendelea kumiminika kambini mkoani Kigoma, Rais Magufuli amemuagiza waziri wa mambo ya nje, ushirikiano wa kimataifa, Afrika Mashariki na Kikanda, Dr Augustine Mahiga, kufufua maongezi ya Amani na mawaziri wenzake wa Afrika Mashariki wanaoshughulikia uhusiano wa kimataifa kuhusu mgogoro unaoendelea Burundi.
Habari kutoka Wizara ya Mambo ya ndani zinasema kufikia sasa Zaidi ya Warundi 120,000 wamekimbia makazi yao na kuingia Tanzania.

Dr Mahiga amesema tayari ameanza kuzungumza na Mawaziri wenzake ili kupanga mikakati ya jinsi watakavyoendesha mazungumzo hayo muhimu, kama alivyoagizwa na mkuu wake Dr Magufuli.

Dr Mahiga amesema kuwa ufumbuzi wa kisiasa pekee na sio mtutu wa bunduki, utamaliza mgogoro nchini Burundi. Amesisitiza kuwa wanatafuta Amani kwa maongezi ya pande mbili.

Wengine atakaokutana nao katika kukamilisha jukumu lake ni pamoja na katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dr Richard Sezibera ambaye atakwenda kuzungumza naye Arusha.

Waziri Mahiga pia amesema Umoja wa Mataifa unashughulikia jambo hili kwa ukaribu na ameshazungumza na Balozi wa Marekani nchini juu ya hali ya kisiasa nchini Burundi.

Wakati hayo yakiendelea, mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR-RCS) kupitia mwenyekiti wake Joseph Butiku, nao umeonyesha nia ya kutaka kuwa sehemu ya ufumbuzi wa tatizo la Burundi. Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam wakati wa kumalizia mkutano wa siku mbili uliokuwa na dhumuni la kujadili utatuzi wa matatizo mbalimbali ya kanda ya Afrika Mashariki.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo