Mkuu wa mkoa awatimua kazi watumishi watatu wa Serikali

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo amewasimamisha kazi watumishi watatu wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema kutokana na uzembe wa kupindukia baada ya kuhusika kuhujumu mradi wa maji unaojengwa na kampuni ya china Civil Engineering Construction Company ya China na kusimamiwa na mhandisi mshauri kampuni ya Cowi Consultant ya jijini Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni ishirini.

Watumishi waliosimamishwa kazi na mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza, ni kaimu meneja wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Mhandisi Nestory Kabete, kaimu afisa ardhi Richard Pungu na mkuu wa idara ya mipango miji Wilson James, ambapo sambamba na kusimamishwa kazi kwa watumishi hao pia mulongo ameagiza watumishi wa kitengo cha ardhi na wanasheria wa halmashauri hiyo kuhamishwa ndani ya wilaya hiyo baada ya kuonekana wanashirikiana kwa namna moja au nyingine na watendaji wa sekta nyingine katika mikakati ya kujipatia fedha kwa njia ya fidia.
 
Hata hivyo Mulongo ameamuru nyumba ya kisasa ya aliyekuwa kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema Pamphil Masashua na wengine waliojenga kwenye njia ya mradi wa maji kubomolewa mara moja ili kuruhusu ujenzi wa mradi huo kuendelea ili uweze kukamilika Februari mwakani kama ulivyopangwa.
 
Kaimu meneja wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira wilayani Sengerema Mhandisi Nestory Kabete alipobanwa maswali na mkuu wa mkoa alishikwa kigugumizi. 
 
Mulongo amemuagiza katibu tawala wa mkoa huo kufanya mabadiliko ya kuwaondoa watu wa ardhi na sheria na kuwapeleka sehemu zingine na kuhakikisha aliowasimamisha kazi wanapewa barua zao haraka, sambamba na kumtaka katibu tawala huyo kuwapeleka wahandisi wa maji kutoka mkoani kwenda kusimamia mradi huo pamoja na kufanya utafiti ili kubaini watu wengine waliojenga juu ya bomba kubwa la maji ambapo ameagiza kupata mrejesho ifikapo Desemba 10 mwaka huu.
 
Awali watumishi hao kwa nyakati tofauti walishindwa kutoa majibu ya kuridhisha kwa mkuu wa mkoa juu ya mradi huo na badala yake walianza kusingizia mvua zinazonyesha kwamba ndizo zinazokwamisha mradi huo kukamilika sanjari na baadhi ya wananchi waliojenga juu ya bomba la maji na wengine kudai fidia.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo