Meya wa CHADEMA Mbeya "ahamia" kwa Magufuli

MEYA mpya wa Jiji la Mbeya kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mchungaji David Mwashilindi, ameahidi kuweka pembeni itikadi za kisiasa na kumuunga mkono Rais wa Jamhuriya Muungano, Dkt. John Magufuli.


Mchungaji Mwashilindi ambaye ni Diwani wa Kata ya Nzovwe, alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 34 ambapo mshindi wa nafasi ya Naibu Meya ni Mchungaji Daud Ngogo, pia kutoka CHADEMA.


Wachungaji hao wote walionesha kukerwa na siasa za chuki zenye lengo la kuleta ubaguzi na kukwamisha maendeleo ya wananchi.


Akizungumza baada ya kushinda nafasi hiyo, Mchungaji Mwashilindi alisema kazi ya kwanza ambayo ataanza nayo katika jukumu alilonalo ni kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli kupitia kauli mbiu yake inayosema "Hapa Kazi Tu".


Alisema kwa kufanya hivyo, anaamini jiji hilo litapata maendeleo ya haraka akitilia mkazo umuhimu wa wannchi kufanya kazi, siasa baadaye ili kufikia malengo yanayokusudiwa.

"Baada ya kuisha michakato yote ya uchaguzi, kilichobaki ni kuona wana Mbeya wanapata maendeleo makubwa, wakati wa kufanya siasa umepita kinachotakiwa sasa ni kufanya kazi za kuhudumia wananchi bila ubaguzi wowote," alisema Mchungaji Mwashilindi.

Kwa upande wake, Mchungaji Ngogo alisema ataitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu, upendo na uaminifu bila ubaguzi wa kidini, chama au rangi bali atafanya kazi ya kuamsaidia Meya.

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Meya kwa tiketi ya CCM, Kephas Mwasote, alikubali matokeo ya uchaguzi huo na kuahidi kumuunga mkono Meya aliyeshinda bila kujali itikadi ya chama chake ili wana Mbeya waweze kupata maendeleo.

Mgombea nafasi ya Naibu Meya kwa tiketi ya CCM, Pantaleo Shiyo, naye alikubali matokeo akisema idadi ndogo ya kura alizopata ndiyo idadi kamili ya madiwani wa chama chake na kuahidi kutoa ushirikiano kwa washindi ili kuchochea maendeleo.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Quip Mbeyela, baada ya kuwatangaza washindi alisema kinachotakiwa sasa ni viongozi hao kuliongoza jiji hilo kwa mujibu wa taratibu, kanuni.


"Msifanye kazi zenu kwa misukumo ya kisiasa ili msilete malumbano yasiyo na maana kwa maslahi ya wananchi," alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa jiji hilo ambaye pia ni Katibu wa baraza hilo, Dkt. Samwel Lazaro, aliwataka madiwani hao kuhakikisha wanasoma kanuni na miongozo ya utumishi wa nafasi zao.

Alisema vyama vya siasa vinatumika kama njia ya kupata uongozi wa kisiasa baada ya hapo, kinachotakiwa ni kuwatumikia wananchi. 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo