WATU
wanne wamefikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kuua ng’ombe 151 wenye
thamni ya Sh milioni 60.4, mali ya mfugaji, Shabani Kidaini.
Watu hao, wote wakazi wa Turiani wilayani Mvomero mkoa wa Morogoro, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa huo.
Waliopandishwa
kizimbani na kusomewa mashtaka hayo na wakili wa Serikali, Teodora
Mlelwa, mbele ya hakimu Agripina Kimaze, aliwataja washtakiwa hao ni
Ally Ramadhani (64), Mussa Salumu (46), Mathew Daniael (46) na Imanuel
Dismas (42) .
Mwanasheria
huyo wa serikali alidai kuwa washtakiwa hao bila kibali halali huku
wakijua kufanya hivyo ni kosa waliwaua ng’ombe hao kwa kuwakatakata na
mapanga sehemu mbalimbali za miili yao. Washtakiwa hao kwa pamoja
walikana mashtaka hayo na kurudishwa rumande baada ya kushindwa
kukamilisha masharti ya dhamana zao.
Mahakama
hiyo iliwataka kila mmoja kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye
thamani ya Sh milioni 15. Kesi hiyo itatajwa tena Januari 7, 2016
ambapo upelelezi bado unaendelea.
Katika
hatua nyingine, Michael Kityanga (54) mkazi wa kijiji cha Msangalilo,
Turiani wilayani Mvomero alipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo
mbele ya hakimu Regina Futakamba, kujibu mashtaka matatu yaliyokuwa
yakimkabili. Mashitaka hayo ni kumjeruhi askari, kupora silaha ya askari
na kuharibu mali ambayo ni gari la polisi.
Katika
mashtaka ya kwanza, mwendesha mashtaka ambaye ni mwanasheria wa
Serikali, Veronica Chacha alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo
Desemba 13 , mwaka huu mwaka huu katika kijiji cha Dihinda, Turiani,
wilaya ya Mvomero.
Mwanasheria
huyo alidai kuwa mshtakiwa huyo aliiba bunduki ya kufyatulia mabomu ya
machozi, ikiwa na mabomu ya machozi 10, mali ya Jeshi la Polisi
Tanzania. Alidai kuwa kabla ya kuiba bunduki hiyo, alimjeruhi askari
aliyekuwa akiitumia, Konstebo Peter wa Kituo cha Polisi Dakawa kwa
kumkatakata kwa panga na kumchoma mshale.
Katika
shtaka la pili, mshitakiwa huyo anadaiwa kuwa alimjeruhi askari polisi,
sajini wa upelelezi Mkaze kwa kumchoma mshale mbavuni. Katika mashtaka
ya tatu, mshtakiwa huyo alidaiwa kuharibu mali ambayo ni gari la polisi
aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba PT 0723 kwa kuvunja vioo na
mlango wa gari hilo.
Mshtakiwa
huyo alikana mashtaka yote na kurudishwa rumande kwa kuwa kesi hiyo
kisheria haina dhamana. Kesi hiyo itatajwa tena Januari 6, 2016 na
upelelezi bado unaendelea