Wananchi walioezuliwa nyumba zao na upepo mkali Makete wapatiwa msaada

Wakazi wa kijiji cha Ukange kata ya Lupila wilayani Makete mkoani Njombe, walioezuliwa nyumba zao na upepo mkali ulioambatana na mvua kali mwanzoni mwa mwezi huu, wamepatiwa msaada wa bati 88 na misumari zaidi ya kilo 40 na halmashauri ya wilaya ya Makete

Akizungumza leo hii kijijini hapo wakati akikabidhi msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Daudi Yassin Mlowe amewapa pole wananchi hao huku akisisitiza msaada huo uwalenge wahusika walioorodheshwa kwenye taarifa ya maafa hayo iliyotumwa wilayani

Mkuu wa wilaya amesema katika tukio la ugawaji wa msaada huo usipotumika vizuri utapelekea msaada huo kugeuka kero badala ya kunusuru hali waliyonayo, hivyo kumuagiza mtendaji wa kata ahakikishe kila mtu anapewa mgawo kulingana na mahitaji yake yaliyoorodheshwa kwenye taarifa iliyopo wilayani

"Naagiza mtendaji wa kata, hakikisha unasimamia ipasavyo huu msaada, sio tufike wilayani tuambiwe tena huku kuna tatizo watu hawakutendewa haki, msaada umewaendea watu ambao hawakupatwa na maafa, hakikisha unalisimamia hilo mambo yaende vizuri" amesema Mh. Yassin

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Francis Namaumbo amesema serikali inatambua kuwa ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wake wanaopatwa na maafa wanasaidiwa na hali zao kurejea kama zamani, na ndiyo maana wamewapelekea msaada huo

Amesema msaada huo umetolewa na halmashauri ya wilaya ya Makete kwa kushirikiana na wadau walioguswa wakati taarifa hiyo ikitangazwa na kituo cha redio cha Kitulo Fm kinachomilikiwa na halmashauri hiyo

Katika hatua nyingine kituo hicho cha redio Kitulo Fm kimetoa msaada wa sabuni katoni 3 kwa wananchi hao ambao nyumba zao 35 ziliezuliwa na upepo mkali, kama njia mojawapo ya kuonesha wao binafsi wameguswa na tatizo hilo, licha ya kutangaza na kukusanya misaada mbalimbali kutoka kwa wasikilizaji na hatimaye wakaiwasilisha kwa uongozi wa wilaya

Mwanzoni mwa mwezi huu upepo mkali ulioambatana na mvua uliezua nyumba 35 za wakazi wa kijiji cha Ukange na kusababisha wengine kukosa makazi kwa muda na wengine kukosa makazi mpaka hivi sasa, huku ikitarajiwa masaada huo utakuwa na manufaa kwao
Mkuu wa wilaya ya Makete Mh Daudi Yassin akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ukange(hawapo pichani)
 Mkuu wa wilaya ya Makete Daudi Yassin akikabidhi msaada kwa wakazi wa kijiji cha Ukange Makete


 Mwananchi wa Ukange akishukuru



 Shukrani zikiendelea


Mkuu wa wilaya ya makete Daudi Yassin (kushoto)akizungumza na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Francis Namaumbo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo