Muda mchache baada ya waziri mkuu Mh Majaliwa Kasimu Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi kamishna mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA pamoja na kuwapiga marufu maafisa wakuu wote wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA kusafiri nje ya nchi.
Katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue ametoa tamko hilo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya rais kauli inayoakisi kauli ya rais Dr Magufuli aliyoitoa bungeni mjini Dodoma wakati akizindua bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ana kazi ya kutumbua majipu na kwamba baada ya ziara ya ghafla ya waziri mkuu bandarini rais Dr Magufuli amechukua hatua hii.
Mbali na kusimamishwa kazi kwa kamishna mkuu wa TRA Rished Bade maafisa waandamizi wa mamlaka ya mapato Tanzania nao wakapewa maelekezo ya rais kupitia kwa katibu mkuu kiongozi Balozi Ombeni Sefue.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kufahamu kodi ya serikali italipwaje na baadhi ya makampuni yaliyofunga biashara zake kwa madai ya kufilisika endapo itabainika katika orodha ndeeefu ya makontena zaidi ya 300 yamepita Bandarini bila ya kulipiwa kodi Balozi Sefue amesema watafuatiliwa na kutoa angalizo kwa wale wanaofahamu wamepitisha makontena yao bandarini bila ya kulipia ushuru.