Mwenyekiti wa CCM Iringa agoma kujiuzulu

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu amepuuza shinikizo toka kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho, Iringa Mjini, linalomtaka aachie ngazi kwa tuhuma kwamba amechangia chama hicho kipoteze jimbo na kata 14 kati ya 18 za Iringa Mjini.

Pamoja na Msambatavangu, wengine wanaotakiwa kuachia ngazi kwasababu ya tuhuma hiyo ni Mwenyekiti wa UVCCM Iringa Mjini, Kaunda Mwaipyana na Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Mkwawa, Salum Keita.

Mbali na viongozi hao, wanachama hao wamemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kwa mamlaka aliyopewa na Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania ahakikishe, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Iringa Mjini anaondolewa kazini kwa kuwa ameshiriki kuvuruga uchaguzi katika jimbo hilo.

Wakati Jesca, Kaunda na Keita wanatuhumiwa kutumia nafasi zao kuwashawishi wapiga kura wa Iringa Mjini kutowachagua wagombea wa CCM katika ngazi ya udiwani, ubunge na urais, Msimamizi wa Uchaguzi anatuhumiwa kutupilia mbali ombi la chama hicho na mgombea wake lililotaka kura za ubunge za jimbo hilo zihesabiwe upya.
Msimamizi huyo wa uchaguzi ambaye majira ya saa nne usiku ya Jumatatu ya Oktoba 26, alishikiliwa na Polisi kwa muda anatuhumiwa na CCM kufungua baadhi ya maboksi ya kura zilizokwishapigwa akiwa pamoja na wanachama nane wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); tuhuma ambazo kaziknusha kwamba si za kweli.
 
Tuhuma nyingine kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivikaribuni na Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga inahusu kuchelewa kupata taarifa ya marudio ya uchaguzi katika kituo cha Ipogolo C kilichovamiwa na watu wasiojulikana Oktoba 25 na kuibiwa na maboksi mawili ya kura wakati zoezi la uhesabuji kura likiendelea.

Mtenga alisema jambo lingine wanalolilalamikia kujitokeza Oktoba 25 wakati wa upigaji kura ni lile linalohusu mawakala wake kuzuiwa kutumia simu wakati kuna ushahidi wa baadhi ya mawakala wa Chadema kuruhusiwa kutumia mtandao huo wa simu.
 
Akikanusha madai ya CCM dhidi yake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo alisema; “ninaifanya kazi yangu kwa weledi mkubwa na kwa kuzingatia sheria za nchi na sheria zote za uchaguzi.”

Alisema hakuna wakala aliyeruhusiwa kutumia simu katika kituo cha kupigia kura kama taratibu zinavyotaka na akazungumzia utaratibu wa kisheria uliotumika kuwapata wasimamizi wasaidizi ambao alisema hawapatikani kwa itikadi zao za vyama.

Kuhusu kukamatwa na Polisi, Sawa alikiri kuitwa na Polisi kwa mahojiano baada ya kuwepo kwa tetesi zilizomuhusisha yeye na maafisa wengine wa tume na wanachama wa Chadema kufungua maboksi ya kura na kuzihesabu kura hizo bila wawakilishi wa vyama vingine kuwepo.

Sawa alisema madai hayo sio ya kweli na kwamba wakati tukio la kuchukuliwa na Polisi likitokea walikuwa wakiendelea kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kutuma NEC matokeo ya kura za rais.

Naye Msambatavangu alisema shinikizo la kikundi cha wanachama wa Iringa Mjini wanaomtaka ajiuzulu linalotokana na majungu, fitina na vikundi vya uasi vinavyoanzishwa na baadhi ya viongozi ndani ya chama  kwa lengo la kulinda maslai ya watu fulani.
“Hivi inawezekaneje mimi na hao wachache tunaotajwa, tukavumiliwa katika kipindi chote cha kampeni tufanye kazi ya kikihujumu chama mpaka baada ya kupoteza jimbo na kata ndio tuseme, wakati kazi hiyo ya kukihujumu chama inafanyika wana CCM na viongozi wengine walikuwa wapi, maana CCM ina mtandao mpaka ngazi ya balozi” alisema.
Alisema kuna njama za kumchafua yeye na viongozi wengine ndani ya chama hicho kwa maslai ya watu fulani kwasababu kuna blanda zilifanyika kinyume na utaratibu kabla ya mchakato wa kura za maoni.
Msambatavangu alisema kama angekuwa mtaalamu wa kutumia hujuma zinazodaiwa na wanachama hao, isingekuwa rahisi kwake kushindwa kura za maoni za kuwania nafasi hiyo ya ubunge dhidi ya aliyekuwa mgombea wao Frederick Mwakalebela.
“CCM Iringa Mjini ina wanachama 26,000; sasa kama nilishindwa kutumia hujuma waanazosisema kuwashawishi wanachama hao wanipigie kura wakati wa kura za maoni, ninawezaje kumsaidia kwa hujuma hizo hizo Mchungaji Msigwa ashinde ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa kupata kura zaidi ya 43,000,” alisema.
Jesca alihoji kwanini wanachama hao wasishinikize viongozi wa wilaya na kata walizopoteza ndio waondoke na badala yake wanamnyoshea kidole yeye huku wakijua yeye ni kiongozi wa mkoa ambaye majimbo yote saba ya uchaguzi yako chini yake.
Alisema katika mchakato wa uchaguzi huo ametumia fedha zake, rasilimali zake na umaarufu wake kukiimarisha chama katika majimbo yote ya mkoa wa Iringa na katika kampeni za Iringa Mjini alifanya mikutano ya kata kwa kata sambamba na mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mwakalebela.
Akizungumzia matokeo yaliyoipa ushindi Chadema, Jesca alisema; “mimi binafsi matokeo ya majimbo yote saba ya uchaguzi mkoani Iringa yakiwemo ya jimbo la Iringa Mjini nimeyapokea na kama kuna taratibu zingine za kuyapinga matokeo hayo tufuate sheria.”
Alisema CCM inatakiwa kufanya tathmini ya kina ya uchaguzi katika jimbo la Iringa Mjini na mengineyo kwa kutumia vikao halali vya chama ili amani iliyopo isivurugike kwasababu za majungu.
Alisema kama kuna malalamiko ya kwenda mahakamani, polisi au kwenye chama, wanachama wote wa CCM wanatakiwa kutuliza akili na kufuata taratibu ili wajipange upya kwa ajili ya kukijenga chama hicho na kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Souce-Bongo leaks


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo