Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini
(CCM), Frederick Mwakalebela amefungua kesi kupinga ushindi
wa Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ruth
Massama alisema juzi kuwa kesi hiyo namba 5 ya mwaka 2015
ya kupinga matokeo, imesajiliwa rasmi Oktoba 30.
Katika shauri hilo, Mwakalebela anawatuhumu Mchungaji Msigwa na msimamizi wa uchaguzi wa
jimbo hilo, Ahmed Sawa kukiuka taratibu kanuni na Sheria ya Uchaguzi na kuchangia yeye kupata
matokeo mabaya.
Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Mchungaji Msigwa anayedaiwa kufanya kampeni siku ya
uchaguzi kwa kuvaa kofia yenye nembo ya M4C ikiwa na picha za vidole viwili, alama
zinazotumiwa na Chadema.
Pia, Mwakalebela anamtuhumu msimamizi wa uchaguzi kwa kuanza kujumlisha matokeo akiwa
na mtuhumiwa wa kwanza pamoja na mawakala wa mtuhumiwa huyo, bila yeye kujulishwa wala
kushirikishwa.
Katika dai lake la tatu, Mwakalebela analalamikia kuzuiwa kuingia kwenye kituo cha kupigia kura
kilichopo Mtaa wa Dabodabo, Kata ya Ilala wakati mgombea mwenzake wa Chadema aliruhusiwa
kuingia bila pingamizi.
Mwakalebela ameambatanisha madai hayo pamoja na barua yake ya Oktoba 25 aliyoituma kwa
msimamizi wa uchaguzi akizuia kazi ya kutangaza matokeo kuendelea, huku akitoa sababu tano
zilizomsukumu kufanya hivyo.
Akitoa ufafanuzi wa kesi hiyo, Massama alisema taratibu zinawataka baada ya kufungua kesi za
uchaguzi, kuwajulisha walalamikiwa na kuweka maelezo kwenye mbao za matangazo kwa siku 14
ili kusubiri kama kutakuwa na pingamizi.
Pia, chama hicho kinajipanga kufungua kesi ya kupinga ushindi wa madiwani wa Chadema wa
kata zilizopo kwenye jimbo hilo kwa kuwa kuna kasoro zinazolalamikiwa.
Katika Uchaguzi Mkuu, Mchungaji Msigwa alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 43,154
dhidi ya 32,406 alizopata Mwakalebela.
Wagombea wengine ni Chiku Abwao wa ACT Wazalendo aliyepata kura 411, Daudi Masasi wa ADC
(123), Paulina Mgimwa wa Chausta (66) na Robert Kisinini wa DP (56).
Wakati huohuo, katibu wa Chadema wa Mkoa wa Njombe, Alatanga Nyagawa amesema chama
chake kinakamilisha utaratibu wa kisheria wa kukata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi katika
majimbo ya Njombe Kusini na Makambako.
Nyagawa alisema hatua hiyo inakuja baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi
katika majimbo hayo kwa kile alichodai kuwa kulikuwa na hujuma zilizofanywa na wapinzani wao,
hivyo kukosa ushindi.
“Siyo kwamba maeneo mengine hatukufanyiwa uhuni, lakini katika majimbo hayo tunatarajia
kukata rufaa mahakamani kwa kuwa tumefanyiwa hivyo mchana kweupe,” alisema Nyagawa.