Aliyegombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Singida Mashariki, Jonathan Njau, amepinga ushindi wa Tundu Lissu (Chadema), akimtaka Msimamizi wa jimbo hilo, Mohammed Nkya, kuruhusu upya uhesabuji wa kura ili kuondoa utata wa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mwishoni mwa wiki, Njau alisema iwapo msimamizi huyo atashindwa kutekeleza ombi hilo, hatakuwa na njia nyingine zaidi ya kwenda mahakamani kuhoji matokeo hayo.
Katika uchaguzi huo, Lissu alitangazwa mshindi, baada ya kujizolea kura 24,874, akifuatiwa na Njau kwa kura 18,393, huku Vedatus Muna, wa ACT-Wazalendo akipata kura 241 na Msafiri Sprian, wa Chama cha Wananchi (CUF), akiambulia kura 85.
Njau alisema kuwa ili haki ipatikane, anaomba uhesabuji kura ufanywe upya kwa madai kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alikiuka kanuni na baadhi ya vifungu vya sheria za uchaguzi.
Alidai kuwa kanuni inamtaka msimamizi wakati wa kuhesabu kura kuhakikisha masanduku yote yamepokelewa, lakini hakufanya hivyo, hali inayotia shaka kwa matokeo aliyotangaza.
Alilalamikia pia ujumulishaji wa kura akidai lazima ufanywe kwa kufuata matokeo ya kura za kituo kwa sababu kila kituo kilikuwa na sanduku lake.