Waziri Kebwe naye atangaza kupinga matokeo mahakamani

Siku chache tu baada ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii dk Stephen Kebwe kubwagwa na mgombea wa Chadema katika uchaguzi wa wabunge jimbo la Serengeti Mkoa wa Mara,amesema anakata rufaa. 

Katika uchaguzi huo uliowashirikisha wagombea watano mgombea wa chama cha Chadema Marwa Ryoba aliwabwaga wote kwa kura 40059 ,dk Kebwe Ccm(39232),Burito Thomas Act Wazalendo(1445) Mosena Nyambabe Nccr Mageuzi (408)na Imakulata Mniko Cuf(328). 

Akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu Dk Kebwe alisema hakubaliani na matokeo hayo kwa kuwa alihujumiwa na msimamizi wa Uchaguzi kwa kushirikiana na mgombea aliyeshinda. 

Hata hivyo Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo Naomi Nnko akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu alisema,anashangazwa na kauli hizo kwa kuwa yeye hakuwa mpiga kura bali msimamizi na hakuna malalamiko yaliyotolewa na mawakala kuwa wamehujumiwa.

 “Alinifuata ofisini kwa vitisho sana kuwa mimi nimemhujumu kwa kumbeba mpinzani na kuwa nitamtambua….mimi sijabeba mtu,nilikubali hoja yake ya kutaka kuhesabu upya ili kujiridhisha lakini yeye kwa kushauriana na wakala wake na mimi akaniita nje alimwagiza wakala nikatangaze matokeo ili kuepusha vurugu toka kwa wananchi waliokuwa wamezingira ofisi hiyo,”alisema. 

Dk Kebwe alisema “hapa naelekea ofisini Dodoma kikazi ,lakini pia nitakutana na Mwanasheria wangu ili tuandae namna ya kufungua kesi Mahakama kuu kupinga matokeo hayo maana uchaguzi ulitawaliwa na dosari nyingi….watu wasio raia Wakisii walipiga kura”alisema. 

Alisema maeneo ambayo anadai walipiga kura ni pamoja na kata za Manchira,Magange,Ring’wani na Kyambahi,na kuwa zoezi hilo liliratibiwa vema na mtandao wa watu wandani na nje ya wilaya kwa kushirikiana na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo. 

Akizungumzia madai ya watu wasiokuwa raia kupiga kura,Nnko ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alisema,hilo si suala lake bali uhamiaji,”nilibandika daftari kwa wiki nzima ili wananchi waone majina hayo,wakazi wa maeneo hayo hawakuweka pingamizi ,haya yeye ,wakati wa kupiga kura wakala wake alikuwa kila kituo hawakuwawekea pingamizi,inakuwaje sasa nitupiwe lawama?”alihoji. 

Hata hivyo Dk Kebwe alibainisha dosari nyingine ikiwemo ya wakala wa CCM waliokimbia na maboksi ya kura katika vituo Machochwe likiwa na kura 120 za Chadema lkini baadae walidai zimepatikana na kujaza,katika kata ya Manchira wakala alikimbia baada ya kuona diwani wake ameshindwa na kuibua vurugu. 

Alipotakiwa kufafanua sababu za kuhujumiwa na anaowatuhumu alisema lengo lilikuwa ni kumwangusha ili kumdhoofisha kisiasa”kuna watu wanataka kugombea mwaka 2020 wameona nguvu yangu inawatisha ,wakashirikiana na msimamizi na wapinzani kunihujumu”alisema. 

Alisema baadhi ya matokeo ya kata ya Nyamoko yalicheleweshwa makusudi ili kupika takwimu ambazo zilimpa ushindi Marwa Ryoba,”nilikuwa naongoza ndipo wakacheza faulo hizo kwa makusudi na yalipoletwa ndipo ikaonekana nimezidiwa”alisema. 

Kwa upande wake aliyekuwa mgombea udiwani kata ya Ikoma Sospeter Nyigoti akizungumzia uchaguzi huo alisema hapakuwa na hujuma zaidi ya kuwa timu ya CCM haikujipanga vizuri toka ngazi ya wilaya hadi chini. 

Nyigoti ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mwenyekiti wa CCM wilaya na Katibu wa chama hicho wilaya,alisema ubinafsi na kutokushirikiana vizuri kulitoa mwanya kwa wapinzani kushinda maeneo mengi ikiwemo Ubunge. 

Naye Mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Taifa (NEC)wilaya hiyo Chandi Marwa alisema ,ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 na 2010 za ujenzi wa barabara ya lami na uwanja wa ndege kutokutekelezwa ni chanzo cha wananchi kuwapa upinzani.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo