Waislamu nchini wametaka kuundwa Tume ya Uchunguzi ya Hijja kutokana na vifo vya mahujaji vilivyotokea mwaka huu wakati wa Ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia.
Waislamu hao wametaka tume hiyo ishirikishe nchi zote ambazo mahujaji wake wamefariki katika hijja ya mwaka huu walipokuwa wakimtupia jiwe shetani eneo la Minna Saudi Arabia.
Wakizungumza kwa mwavuli wa Muungano wa Waislamu wa madhehebu mbalimbali nchini, Masheikh hao wa taasisi tofauti wametoa tamko ambalo pia linapendekeza Serikali ijiridhishe na hali ya usalama ilivyo huko Hijja kabla ya kupeleka mahujaji.
Akitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam, Sheikh Ghauth Nyambwe, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Al Mustapha, anaelezea mapendekezo yao ya kutaka Tume ya Uchunguzi kuhusu maafa ya Minna ikiwemo kuangalia hali ya usalama pamoja na utaratibu uliotumika hijja.
Hadi sasa zaidi ya mahujaji elfu nne kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanasadikika kufariki dunia katika Hija ya mwaka huu iliyofanyika Makka, lakini idadi kamili ya Watanzania waliofariki bado haijajulikana.
Sheikh Abdulmajid Almas, Msomi wa Teolojia ya Dini ya Kiislamu, ni miongoni mwa mahujaji wa Tanzania aliyekwenda Hija mwaka huu na kushuhudia tukio la maafa kwa mahujaji.
Vifo vya mahujaji katika Ibada ya Hija vimekuwa vikitokea na tukio la mwaka huu limeibua maswali mengi miongoni mwa Waislamu kuhusu kipaumbele cha usalama wakati wa ibada hiyo.
Sheikh Mulaba Saleh, Mwalimu na Mtafiti wa masuala ya Kiislamu, anaelezea takwimu za maafa ya mahujaji katika hija kuanzia mwaka 1972 hadi sasa.
Tukio la hija ni moja ya nguzo muhimu za Uislamu, ambalo hufanyika mara moja kila mwaka katika miji mitakatifu ya Makka na Madina, Saudi Arabia.