Taarifa kamili ya kuahirishwa kwa uchaguzi Zanzibar iko hapa

Na Mwandishi wetu, Zanzibar
TUME ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) , imefuta na kuhairisha matokeo yote ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kutokana na kujitokeza kwa kasoro mbali mbali za ukiukaji wa sheria na kanuni za uchaguzi Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha alisema kuwa kutokana na kasoro mbali mbali zilizojitokeza katika uchaguzi huu na kusababisha vikwazo mbali mbali zilivyosababisha ZEC kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.
Jecha alisema kuwa uchaguzi huo katika kipindi cha kampeni za uchaguzi ulionekana kuwa shwari licha ya kujitokeza kwa kasoro ndogo ndogo hasa zilizotokana na hamasa za wafuasi wa vyama vya siasa, na kutatuliwa kwa hekima na busara za tume.
Mwenyekiti huyo alizitaja kasoro zilizosababisha kufutwa na kuhairishwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, alisema ni pamoja na baadhi ya mawakala wa vyama kubeba visanduku vya kura na kwenda kuhesabia kura hizo nje ya vituo husika pamoja na baadhi ya makamishna wa tume waliochaguliwa kuwakilisha vyama vyao kufanya kazi za kisiasa ndani ya tume na kufikia hatua ya kutaka kupigana.
Alisema kasoro nyingine ni pamoja na idadi ya kura zilizopigwa kuwa nyingi kinyume na idadi ya watu waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura huko Pemba kwani wananchi wengi walisusia kwenda kuchukua vitambulisho vya kupigia kura.
Alifafanua kuwa kwa upande wa vituo vya Pemba kulijitokeza kwa baadhi ya vijana walionekana kuandaliwa na vyama vya siasa waliovamia vituo kwa kuwatisha na kuwapiga watu waliohisi siyo wafuasi wao, pamoja na kuwepo na malalamiko mbali mbali ya vyama vya siasa kutoridhishwa na matokeo ya vituo mbali mbali vya kupigia kura.
Salim aliendelea kuzita kasoro hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya fomu za matokeo ya vituo vya kupigia kura kwa upande wa Unguja na Pemba kuonekana namba za mwanzo zimefutwa na zimeandikwa mpya, hali iliyoonesha kuwa kumfanyika udanganyifu katika vituo hivyo.
Aidha aliitaja kasoro nyingine kuwa ni pamoja na baadhi ya vyama vya siasa kupokonya kibabe mamlaka ya Tume ya uchaguzi na kujitangazia wenyewe matokeo kuwa wameshinda huku wakiishinikiza tume ifuate matakwa yao jambo ambalo ni kosa la jinai kisheria.
“Kutokana na kasoro hizo ZEC imekaa chini na kutathimini pamoja na kujiridhisha kwa kina na kuona kuwa sheria na kanuni za uchaguzi Zanzibar imekiukwa kwa makusudi, hivyo kwa mamlaka niliyopewa kikatiba nahairisha uchaguzi na kufuta matokeo yote na kuona kuna haja ya kufanyika uchaguzi mwingine ambao utakuwa huru na wa kidemokrasia ambapo tutataja tarehe nyingine ya kufanyika uchaguzi huo.
Hatuwezi kuona nchi inaingia katika migogoro na sisi tukaacha kuchukua maamuzi eti kwa kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wanataka yafuatwe matakwa yao hata kama ni kinyume na sheria na katiba ya nchi haiwezekani tume kufuata matakwa ya watu ama chombo kingine wakati hii ni tume huru.”, alisema Salim na kuongeza kuwa kasoro hizo zisingeweza kuachwa kwani nchi ingweza kuingia katika machafuko kutokana na maslahi ya wachache.
Nao mawakala mbali mbali wa vyama vya kisiasa waliokuwa wakisimamia masuala ya uchaguzi nchini kwa nyakati tofauti ambao walikusanyika katika kituo kikuu cha taarifa cha tume hiyo huko katika hoteli ya Bwawani Zanzibar, walilaumu tume ya uchaguzi Zanzibar kutoa uamuzi wa jumla bila ya kuviwajibisha vyama vilivyohusika moja kwa moja kuvuruga utaratibu wa uchaguzi huo.
Walisema kuwa ili kunusuru nchi kuingia katika migogoro ni lazima tume ya uchaguzi iharakishe uchaguzi mwingine kwa lengo la wananchi kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kuwachagua viongozi wanaofaa.
” Sisi tunashangaa sana kuona hapa Zanzibar vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi mkuu huu ni vingi lakini leo hii vyama vinavyoonekana vinailamisha tume ifanye maamuzi ya kuwatesa wananchi ni CUF na CCM kwani toka mwanzo ndiyo wanaotuharibia uchaguzi wetu”, walisema mawakala hao.
Aidha walieleza kuwa tume ya uchaguzi Zanzibar ni bora ikaacha kufanya mukhari kwa baadhi ya vyama vya siasa vinavyovunja katika ya nchi kwa makusudi kwani bado kuna maisha ya wananchi wengi wanaohitaji hali ya amani na utulivu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo