Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Iringa mjini Ahmed Sawa amemtangaza mchungaji Peter Simon Msigwa kuwa mshindi wa kiti cha ubunge wa jimbo la Iringa mjini baada ya kuwashinda wapinzani wake kwa kura 43,154 katika jumla ya kura 76,216 zilizopigwa huku mpinzani wake Fredrick Mwakalebela wa CCM akipata kura 32406,Chiku Abwao wa ACT Wazalendo aliyepata kura 411.
Matokeo hayo yametangazwa baada ya msuguano mkali baina ya pande mbili yaani upande wa chama cha mapinduzi CCM na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Iringa mjini kufuatia kupotea kwa masanduku mawili kutoka katika kituo cha kupigia kura Ipogolo C ambapo baadae tume iliamua upigaji kura katika kituo hicho urudiwe kuondoa utata na sintofahamu iliyokuwepo.
blog hii imezungumza na mchungaji Peter Msigwa ili kujua nini kinafuata mara baada ya ushindi huo wa kishindo ambao umekipa ushindi chama cha Chadema kwa kupata viti 14 vya udiwani katika jumla ya kata 18 za manispaa ya Iringa hivyo kutoa nafasi kwa chama hicho kuunda halmashauri kwa mara ya kwanza.
Awali jeshi la polisi mkoani Iringa lililazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya wafuasi wa chama cha Chadema waliokuwa wanajikusanya kwenda kusikiliza matokeo ya ubunge lakini baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo kundi kubwa la wafuasi wa Chadema lilivamia halmashauri hiyo gafla wakishangilia ushindi huo huku baadhi yao wakielezea furaha yao.