HATIMA ya Mawaziri waandamizi wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona, waliohukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh. milioni tano kuachiwa au kuendelea na kifungo imejulikana leo baada ya kupunguziwa adhabu hiyo na sasa watatumikia kifungo cha miaka miwili kati ya miaka mitatu waliyokuwa wamehukumiwa na Hakimu Mkazi Kisutu Julai mwaka huu.
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo Oktoba 2, 2015, imetoa hukumu ya rufaa dhidi ya mawaziri hao ambapo Jaji Projest Rugazia, amekubaliana na hoja kwamba kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyowatia hatiani kwa matumizi mabaya ya Ofisi na kwa mujibu wa kifungo cha 35 cha adhabu PC ambacho Mahakama ilikitumia walipaswa kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili na si miaka mitatu.
Aidha, amekubaliana na hoja za warufani hao na kuwa walikuwa wameadhibiwa mara mbili kwa kosa moja wakidai kuwa kwa mashtaka ya matumizi mabaya ya Ofisi, shtaka la kuisababishia serikali hasara halikupaswa kuwepo.
Hata hivyo, amesema bado Mramba na Yona wamerudishwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka miwili baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosha kwa kumuondolea mashtaka ya kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni za kigeni.
Wafungwa hao kwa pamoja walikutwa na hatia ya kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa madini ya dhahabu nchini kwa njia zisizo halali.
