Vyombo vya Habari hapa nchini vimeelezwa kuwa na dhamana kubwa ya kuuelimisha umma katika kufanikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, katika kuliepusha taifa na viashiria vyote vya uvunjifu wa amani.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC,Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema hayo wakati alipokutana na wamiliki wa vyombo vya habari jijini Dar es salaam, lengo likiwa kubadilishana mawazo kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu ambapo amesisitiza kwamba Tume inatambua uwezo wa vyombo vya habari katika kufikisha ujumbe kwa umma.
Aidha,Mwenyekiti huyo wa NEC ametoa mwelekeo wa Maandalizi ya uchaguzi ambapo amebainisha kwa kiasi kikubwa yamekamilika ambapo sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ipo katika mchakato wa mwisho wa kuchapisha daftari la wapiga kura baada ya kuweka hadharani lile la awali.
Katika mkutano huo jaji lubuva amebainisha kuwa majimbo mawili yaliyohairishwa uchaguzi wake kutokana na sababu za kufariki kwa wagombea pamoja na madiwani wa kata tano uteuzi wa wagombea utafanyika oktoba 12 mwaka huu kwa vyama husika tu na kuanza kampeni oktoba 13.