Mgombea mwenza wa urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA ),anayewakilisha vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi ( UKAWA) Mh. Juma Duni Haji ameendelea na mikutano ya kampeni za kumnadi mgombea urais wa chama hicho Mh. Edward Lowassa katika mkoa wa rukwa na kuhaidi kuwa UKAWA ikiingia madarakani,serikali itawajengea wananchi wa jimbo la kwela kituo cha afya, barabara na kuwapatia huduma ya majisafi na salama kwa kutumia mapato ya sekta ya madini peke yake.
Akiwahutubia wananchi wa vijiji vya ilemba,mto wisa na muze vilivyoko katika bonde la ziwa rukwa,jimbo la kwela sumbawanga vijijini katika mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi mkuu – mgombea mwenza huyo wa urais wa chadema chini ya mwavuli wa vyama vinne vinavyounda ukawa,Mh. Juma Duni Haji amesema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa bonde hilo la ufa wakiishi maisha ya dhiki na kuwaomba watanzania kumchagua Mh.Edward Lowassa Oktoba 25 mwaka huu ili aweze kubadili hali zao za maisha kwa kuwaletea maendeleo.
Aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la mkanyageni Pemba kupitia chama cha wananchi( CUF ),Mohammed Habib Mnyaa pamoja na mwenyekiti wa chadema mkoa wa Rukwa Zeno Lukoswe wamesema laiti kama serikali ya chama cha mapinduzi ingewekeza katika bonde hilo,lingechangia kukuza utalii na kuongeza mapato ya serikali badala ya kulitelekeza na kusababisha umaskini kwa wakazi wanaoishi ndani ya bonde hilo.