Jeshi la polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi Wa kijiji cha Itukutu kata ya Ulemo waliofunga barabara mkoani Singida baada ya basi la kampuni ya City Boy kugonga watu watatu usiku huu majira ya saa mbili na nusu
Kwa mujibu wa mwandishi wa mtandao huu Kadama Malunde ambaye yupo eneo la tukio amesema tarifa za awali zinasema miongoni mwa watu hao watatu waliogongwa wawili wamefariki dunia, ndipo wananchi walipojitokeza na kuziba barabara, huku majeruhi mwingine akikimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi
Basi hilo lilikuwa likitoka Dar Es Salaam kuelekea jijini Mwanza ambapo linadaiwa kuwa katika mwendo kasi na katika harakati za kumkwepa mzee mmoja barabarani ilishindikana likamgonga na kisha kuwagonga watu wengine wawili
hali hiyo ilipelekea wananchi kufunga barabara kwa matawi ya miti na kurusha mawe kwa basi lililosababisha ajali ingawa dereva alifanikiwa kuliondoa eneo la tukio huku mengine yakizuiwa kuendelea na safari
Tukio hilo lilidumu kwa takriban dakika thelathini na ndipo jeshi la polisi lilipofika na kufanikiwa kuwatawanya wananchi hao
Hata hivyo mabasi hayo yameruhusiwa kuendelea na safari