Hali ya mtafaruku iliibuka jana wakati aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani, alipogeuka bondia kwa kumpiga makonde msimamizi wa uchaguzi , Jonathan Mabihya.
Baada ya kutangazwa kushindwa kwa uchaguzi wa marudia wa kura za maoni.
Dk. Kamani amebwagwa na Raphael Chegeni ambaye alikuwa mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, Dk. Kamani alipotakiwa kueleza sababu ya shambulio hilo, hakutaka kueleza na badala yake alisema hakutendewa haki.
Katika valangati hilo, Dk. Kamani alipata hasara baada ya kuvunja miwani yake kutokana na ngumi yake ya mkono wa kulia kumkosakosa msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya ya Meatu.
Wakati Mabihya akitaja jina la Dk. Chegeni kama mshindi, miwani ya Dk. Kamani ilidondoka wakati akimsindikiza kwa konde la mkono wa kulia katibu huyo.
Hali hiyo ilisababisha polisi kuingilia kati ili kuokoa purukushani hiyo na kurudisha hali ya amani.
Vurugu hizo zilizodaiwa kuanzishwa na Dk. Kamani na wafuasi wake, zilisababisha viongozi wa CCM waliokuwa wakisimamia uchaguzi huo kabla ya matokeo kutangaziwa kuondoka ofisi za chama hicho wilaya ya Busega wakisindikizwa na polisi.
Mawaziri ambapo mpaka sasa wamebwagwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Mathias Chikawe, (Mambo ya Ndani), Gaudentia Kabaka (Kazi na Ajira) na Dk Seif Rashid (Waziri wa Afya) wakati Manaibu ni wa Fedha Adam Malima, Maji, Amos Makala, na Makongoro Mahanga wa Kazi na Ajira.
