JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA
USTAWI WA JAMII
|
Ugonjwa wa Ebola
umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo hadi sasa nchi tatu
ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone,
zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya. Aidha, mpaka tarehe 19 Julai 2015,
idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 27,705 na vifo
11,269. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa
huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa udhibiti
wa ugonjwa huu wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.
Historia ya Mgonjwa
Mnamo tarehe 9 Agosti
2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu
alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni akiwa na dalili za
kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi, macho na
masikio. Vile vile alikuwa na dalili za kuchoka na mwili kuwasha. Mgonjwa huyu
hakuwa na homa. Alipata matibabu katika hospital hiyo na kwa bahati mbaya mnamo
tarehe 10 Agosti, 2015 mgonjwa huyu alifariki dunia. Mgonjwa huyu alikuwa hana
historia ya kusafiri kutoka nje ya mkoa wa Kigoma wala kutembelewa na mtu
aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.
Mgonjwa huyu
alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika kambi ya
Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa mmojawapo wa wakimbizi
waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida chini ya Shirika la Kimataifa
linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9
Agosti 2015.
Hatua zilizochukuliwa
- Mgonjwa huyu alipatiwa matibabu katika hospitali ya
Maweni Kigoma mpaka mauti ulipomkuta.
- Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu
wa mgonjwa huyu, pamoja na wahudumu wa Afya waliomuhudumia mgonjwa huyu
kuona kama wataonyesha dalili zinazofanana na ugonjwa aliokuwa nao mgonjwa
huyu. Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu
mwingine, aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
- Sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa
kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha
ugonjwa huu.
- Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya
uangalizi wa Afya mkoa, kwa kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za
kuzuia maambukizi.
Hitimisho
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda
kuwahakikishia wananchi kuwa mpaka sasa, hakuna uthibitisho wowote kuwa mgonjwa
huyu amekufa na ugonjwa wa Ebola. Aidha kwa kuwa ugonjwa bado unaendelea nchi
za Afrika Magharibi, Wizara inazidi kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za
kujikinga na ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwa ni pamoja
na
- Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo,
jasho, kinyesi, machozi na majimaji
mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa
mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola
kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
- Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa
na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa
kituo cha kutoa huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko
ikiwa kifo kitatokea.
- Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza
kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
- Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika
ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye
dalili za ugonjwa wa Ebola.
- Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili
za ugonjwa huu.
- Kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuka kusambaza
ugonjwa ikiwa mtu atakuwa ameshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
- Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.
Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii itatoa taarifa pindi majibu ya maabara
yatakapopatikana.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali – Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii
12 Agosti, 2015