Nape Nnauye (Kushoto) akiwa na Edward Lowassa kabla hajakihama chama cha Mapinduzi
Akizungumza juzi, Nape alisema Lowassa hapendwi na wafuasi wa vyama vya upinzani, isipokuwa alipewa nafasi hiyo baada ya kuinunua kwa viongozi wanaounda umoja wa Ukawa, ambao wana tamaa ya fedha.
“Kila mtu anajua kuwa huyu bwana ameinunua hii nafasi kwa viongozi wa Ukawa, ndiyo maana watu wenye akili zao, wameamua kujiweka pembeni wamewaachia wenyewe na mzigo wao usiobebeka, inashangaza kuwa sisi tunawafukuza mafisadi wao wanawapokea, sasa wakipewa nchi si itakuwa hatari zaidi?” alihoji Nape.
Alisema Lowassa alitumia fedha nyingi kuwarubuni watu wa Ukawa ili wampe nafasi baada ya kukatwa CCM, ndiyo maana baada ya kumkaribisha kundini, hakuna tena kiongozi wa Chadema wala Ukawa anayezungumza kuhusu ufisadi, kwani mlengwa wao mkuu wa miaka yote kuhusu ufisadi alikuwa Lowassa.
“Hivi umeshawasikia tangu ajiunge nao wanazungumza kuhusu ufisadi? Wanaona aibu kwa sababu katika nchi hii, ukitaja fisadi na mafisadi huwezi kumweka kando. Unafikiri Watanzania ni wajinga kiasi kwamba hawaoni huu usanii?” alihoji Nape.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika, wala yule wa Zanzibar Salum Mwalimu hawakuweza kupatikana kuzungumzia madai hayo, jitihada zinaendelea.