SKYNER Ally ‘Skaina’ amekiri kukutana na changamoto ya kuombwa rushwa ya ngono na baadhi ya wazalishaji wa filamu (producers), ili aweze kuonekana kwenye filamu mbalimbali, jambo ambalo anakiri kumkatisha tamaa katika safari yake ya kufika mbali kisanii.
Akibadilishana mawazo na mwandishi wetu hivi karibuni, Skaina ambaye anaendesha maisha yake kupitia uigizaji, alisema kutokana na malezi bora aliyoyapata kutoka kwenye familia na misingi ya kidini, vinamfanya kuwa mwanamke mwenye kujiheshimu na kwamba anaamini katika kipaji halisi na siyo kuhonga rushwa ya ngono.
“Nimewahi kukutana na changamoto ya kuombwa rushwa ya ngono na baadhi ya watengenezaji wa filamu, lakini hakuna hata mmoja aliyefanikiwa, nimelelewa katika familia imara sana, hata misingi ya kidini imenifanya kuwa mwanamke mwenye kujiheshimu, nitaendelea kubana. Kama ipo, ipo tu,” alisema Skaina.