Magufuli Akataa Mawaziri Wazembe......Asema Serikali Yake Haitakuwa na Blaa Blaa

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema serikali yake ya awamu ya tano haitakuwa na blablabla katika utendaji wa kazi na kuonya kuwa waziri atakayeshindwa kutelekeza majukumu yake, ataondolewa ili kupisha wenye uwezo.

Dk.  Magufuli alitoa ahadi hiyo jana, wakati akijinadi kwa wananchi wilayani Nkasi na Kalambo, mkoani Rukwa  akiwa katika siku ya pili ili achaguliwe kuwa rais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Alisema Baraza lake la Mawaziri ni lazima liwe na tofauti kubwa kwani watakuwa watumishi wa watu na siyo mabosi wa watu.

Alisema  waziri atakayeteuliwa katika serikali hiyo, atampima na akiona hawezi kutimiza majukumu yake ipasayo kwa wananchi, lazima aondolewe na nafasi yake ichukuliwe na waziri mwingine mwenye kasi ya kufanya kazi kama yake, vinginevyo atawafukuza kila mara.

Dk. Magufuli ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ujenzi, alisema atafanya hivyo kwa sababu wananchi wanataka matatizo yao yatatuliwe kwa wakati na si kusubiri siku inayofuata.

 “Baraza langu litakuwa la kutetea wanyonge, litafanya kazi za wananchi, nachukia uzembe na nitaonyesha kwa vitendo,” alisema na kuongeza kuwa serikali yake itahakikisha fedha zinapelekwa kwa wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Ifike mahali tunaadhimisha wiki ya maji na maji yapo, wiki ya nyama na nyama zipo, wiki ya Ukimwi na dawa zipo na wiki ya maziwa na maziwa yapo,” alisisitiza.
 
Vilevile, aliwaonya watendaji wazembe akisema hawana nafasi kwani mwendo wake utakuwa ni wa mchakamchaka na hakutakuwa na mapumziko hadi maendeleo yawafikie wananchi. 
 
Mgombea huyo aliahidi kuunda serikali isiyo na kero kwa wananchi wa ngazi zote, wakiwamo wa kipato cha chini, na  itakuwa mkombozi kwa mamalishe na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda kwa kuwa itahakikisha zinafikia mwisho.

Kwa upande mwingine, Dk.  Magufuli aliahidi kuboresha mishahara na maslahi mengine kwa madaktari na wauguzi ili kudhibiti wizi wa dawa za serikali na kuziuza kwa wagonjwa kwenye maduka yao na kusababisha hospitali, vituo vya afya na zahanati kukosa dawa.

“Tunataka hospitali na zahanati zetu ziwe na dawa za kutosha, mwananchi apate huduma nzuri,” alisema.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo