Lowassa Awaonya Polisi


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.

Kutokana na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni takriban kilomita nane.

Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.

“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.

Akizungumzia idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.

Lowassa aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hegue.

“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.

Ampa Wenje kibarua
Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.

Alisema anafahamu Wamachinga, meli ya Mv Victoria, kiwanda kikubwa cha kusindika nyama, reli, ujenzi wa uwanja mkubwa wa ndege, bei ndogo ya pamba na tatizo la umeme.

Kuhusu suala la umeme, Lowassa alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje ni kijana anayefanya uamuzi mgumu kama yeye hivyo alimtaka leo kwenda kwa Meneja wa Tanesco Mwanza ili kujua tatizo, asipopewa majibu ya kuridhisha ampigie simu yeye (Lowassa).

Freeman  Mbowe
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe, alisema nchi nzima kuna msiba wa umaskini kuanzia kwa watumishi wa umma, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wamachinga na mama lishe.

Hata hivyo, alisema msiba huo umesababishwa na kikundi kidogo cha viongozi wachache wanaotumia woga na umaskini huo kuendelea kuwakandamiza wananchi.

Alisema wananchi mkoani Mwanza waliojitokeza kumdhamini Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Haji Duni, ni zaidi ya 100,000, lakini waliojazwa kwenye fomu ni 200 kama kanuni na taratibu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), zinavyotaka.

“Namwambia Mkuu wa Majeshi, asiliingize Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusaidia ushindi wa CCM...vijana watatu wataalam wa kompyuta aliowachukua katika Jeshi la Wananchi na kuwapeleka Nec kwa majukumu maalum ambayo yataisha Novemba 15, amewapeleka kufanya nini?” alihoji.

Aliongeza kuwa: “Namuuliza Jaji Lubuva, hao vijana wa kijeshi uliowapokea ofisini kwako umewapokea kwa kazi gani?...nipo tayari kutoa ushahidi wa taarifa hizi.” 

Alisema ana ushahidi wa namba, majina na vikosi wanavyotoka askari hao pamoja na tarehe waliyoanza kazi Nec.

Twaha  Taslima
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Cuf, Twaha Taslima, alisema kwa mujibu wa sheria, polisi wanapaswa kulinda amani iliyopo na siyo kusababisha fujo kwa kuwapiga mabomu wananchi wanapokusanyika kwa amani.

James Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema polisi wakiendelea kutumia nguvu dhidi ya raia wasio na silaha, wataishia The Hague kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC), Novemba.

Alisema ilani ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa itakayozungumzia malengo ya serikali ya awamu ya tano, itazinduliwa Jumamosi wiki hii sambamba na uzinduzi rasmi wa kampeni.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo