CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam jana kimetangaza majina ya wagombea udiwani katika majimbo 10 ya uchaguzi huku ikiwaengua, Yussuf Manji na Diwani wa Kata ya Jangwani Abuu Jumaa.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alitangaza wagombea wa udiwani kwa tiketi ya CCM wa kata 91 huku kata moja ya Mianzini katika Jimbo la Mbagala uchaguzi wake utafanyika baadaye baada ya ule wa wali kuvurugika.
“ Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ndiyo yenye dhamana ya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya udiwani, baada ya kupokea majina na baadaye kupitia na kuhakiki malalamiko yote,” alisema Simba.
Katika kata ya Mbagala Kuu ambayo Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliongoza katika kura hizo alikatwa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kukosa sifa na nafasi kuchukuliwa na mgombea aliyeshika nafasi ya pili Abubakari Othuman.
Kwa upande wa kata ya Jangwani ambayo wananchi walilalamika Diwani wa kata hiyo, Jumaa kwa kuongoza tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza, jina lake limekatwa na kupitishwa la mgombea aliyeshika nafasi ya pili Abdul Faraji.
Aidha, akizungumza malalamiko ya wanachama wa CCM kata ya Mbagala Kuu ambao walifika ofisini hapo kwa basi maalumu kupinga kuenguliwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida alisema Manji amendolewa kutokana na kukosa sifa.
“ Manji hakutokea kuchukua fomu wala kurudisha fomu, lakini hilo sio tatizo, wakati wa kampeni tuliweka utaratibu wa wagombea kutumia usafiri mmoja kwenye kuomba kura kwenye matawi, Manji hakushiriki. “
Hata wakati wa vikao vya mchujo vya Sekretarieti na kamati ya usalama na maadili ngazi ya kata na wilaya, Manji hakutokea na alipopigiwa simu alijibu amelala.
Alisema kutokana na kutofuata taratibu hizo Manji anakosa sifa za kuwania nafasi ya udiwani, kuwa kura alizopata amezipata kwa hila hivyo sio halali.
“Tulipokaa kwenye mchujo katika sekretarieti na kamati ya usalama na maadili ngazi ya mkoa, Manji pia hakutokea na hapo ndipo yalipokuja malalamiko ya wagombea wenzake kuwa mtu akiwa na fedha anaweza kulala nyumbani kwake, asipige kampeni na akapewa nafasi ya kugombea,” alisema.