Chadema Wilaya ya Bariadi kimedai kunasa kadi 36 za kupigia kura zilizokuwa zimetupwa kwenye gofu la nyumba moja mjini Bariadi.
Hata hivyo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Erika Musika alisema hana taarifa yoyote kuhusiana na kadi hizo… “Nimerudi leo kutoka kwenye Mbio za Mwenge.
Kama kuna tatizo hilo tutawataarifu NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) halafu watatoa majibu.” Chadema kimedai kuwa kadi hizo za kupigia kura (ambazo majina yake tunayo), zilionekana jana katika nyumba karibu na uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mbili zilikuwa za mtu mmoja zenye picha na namba zinazofanana.
Kadi nyingine mbili ni za watu wawili tofauti na zina rangi ya pinki na kijani zenye nembo ya NEC, jambo linalodaiwa kuwa ni njama chafu zinazofanywa kwa lengo la kutaka kukibeba chama kimoja. Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Bariadi, Martin Mogan alidai kwamba kadi hizo zimetengenezwa kwa lengo la maalumu la kukibeba chama kimoja katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Mara ya kwanza jana asubuhi tulipata kadi 21 zikiwa zimetupwa kwenye hilo jumba bovu. Kadi nyingine 15 tulizipata maeneo ya karibu na Benki ya NMB mjini Bariadi zikiwa zimetupwa pia. Tutazipeleka polisi.”
Mogan aliitaka NEC itoe maelezo… kuhusu kadi hizo akisema hizo ni dalili za goli la mkono.
Mwanasheria wa Chadema Kanda ya Serengeti ambaye pia ni mgombea ubunge Jimbo la Bariadi, Godwin Ngwilimi alisema kupatikana kwa kadi hizo kunathibitisha kuwa kuna njama za kuiba kura Oktoba 25.