Chama cha demokrasia na maendeleo, Chadema kimesema kabla ya kumpokea waziri mkuu mstaafu, Mh.Edward Lowassa na kumpatia nafasi ya kugombea urais kupitia vyama vinavyounda UKAWA, kilimuhoji kwa zaidi ya wiki mbili na kujiridhisha kuwa hakuhusika moja kwa moja kwenye ufisadi wa zabuni ya kufuafua umeme wa dharura uliohusisha kampuni feki ya Richmond.
Mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, David Ernest Silinde ameyasema hayo wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa mji wa Tunduma kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika jimbo jipya la uchaguzi la Tunduma.
Silinde ambaye pia ni mgombea ubunge wa jimbo la Momba amesema baada ya kujiridhisha kwa vielelezo kuwa Mh.Lowassa hakuhusika, UKAWA wameamua kumsimaisha kugombea urais huku wakiwataka wale wanaomtuhumu kuwa ni fisadi waende mahakamani.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Tunduma, Frank George Mwakajoka amesema kuwa wananchi wanahitaji mabadiliko na kwamba endapo kura za mgombea urais wa UKAWA, Mh.Edward Lowassa zitachakachuliwa yupo tayari kuhamasisha vijana kutembea kwa miguu kuanzia Tunduma hadi Dar es Salaam kudai haki.
