Rais Kikwete amekamilisha ziara yake katika maeneo yaliathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kwa kuwataka wanaoishi mabondeni kukubali kuhama kutokana na maeneo hayo kuwa hatarishi kwa maisha yao.
Rais ametembelea maeneo mbalimbali ndani ya manispaa ya Kinondoni kwa kuanza na Boko Basiaya na Boko Dawasco na kujionea jinsi ambavyo maji yamejaa ndani nyumba za watu na kusababisha watu kukimbia makazi yao huku akitupa lawama kwa viongozi wa manispaa ya Kinondoni akiwemo mkurugenzi na mhandisi wao kwa kushindwa kufanya njia mbalimbali ili kuondoa maji yaliyotuhama katika makazi yawatu.
Rais alienda mbali zaidi kwa kuwaagiza viongozi hao kubomoa baadhi ya nyumba zinazosababisha maji kutuhama kwa manufaa ya wengine.
Kutokana na hali ilivyokuwa mbaya katika maeneo hayo, rais aliwataka wahandisi kutoa maelezo kwanini wameshindwa kutatua tatizo hilo ambapo mhandisi wa manispaa ya Kinondoni Baraka Mkuya pamoja na kaimu mhandisi wa Dawasco eneo la Boko Bwana Marwa Wambura walionekana kutoa maelezo ambayo hayakumridhisha rais katika kumaliza tatizo.
Baadhi ya wakazi hao wamemwambia rais kuwa kuna baadhi ya watu wamehusika kusababisha hali hiyo huku mama mmoja akimuomba rais kwa masikitiko kuwasaidia maji hayo yaondolewe katika eneo.
Akihitimisha msafara wake katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, rais aliwataka wakazi wa maeneo ya mabondeni wakiwemo wa eneo hilo kukubali kuhama kutokana na maeneo hayo kuhatarisha maisha yao.
Tangu mvua zianze kunyesha jijini zaidi ya watu kumi na mbili wameripotiwa kupoteza maisha huku zaidi ya wakazi elfu mbili wakidaiwa kukosa makazi.