MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Sadifa Khamis Juma, amesema kitendo cha baadhi ya wanachama wanaotaka kugombea urais kuendelea kuchafuana ni dalili mbaya ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika ziara yake ya kikazi wilayani Mwanga wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wake wa hadhara.
Alisema kuchafuana kwa baadhi ya viongozi hakuijengi CCM bali kunaibomoa.
Alisema baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wameonyesha kile alichosema propaganda chafu za kuchafuana na kujengeana chuki za kisiasa.
“Imeibuka tabia chafu ya kisiasa kwa baadhi ya watu kuchafuana hasa wale wanaotajwa katika nafasi ya urais, kwamba fulani amehonga milioni sasa kama na wewe unaweza fanya hivyo acheni kuchafuana,”alisema Sadifa.
Alisema CCM hakikusudii kukata majina ya wagombea watakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
“Kumekuwa na hofu ya wagombea wa nafasi za uongozi hasa ya urais juu ya kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hizo kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, jina la mtu litakatwa tu pale itakapobainika kuna sababu za msingi,” alisema Sadifa.
Alisema CCM imekuwa ikishindwa katika uchaguzi kutokana na makundi ndani ya chama hicho na endapo yatajitokeza tena mwaka huu watarajie ushindi mdogo.