MWANAUME AKIRI MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUMILIKI NYOKA 13 NA KOBE 22

Bw Raphael GaloziMAAFISA wa mahakama ya Kwale wanatarajiwa kuzuru nyumba ya Raphael Galozi ambaye alikamatwa na polisi kwa kosa la kumiliki nyoka 13 na kobe 22 bila ya kibali hii Jumanne.

Haya ni baada ya Bw Galozi kufikishwa mbele ya mahakama hiyo na kukiri mashtaka dhidi yake ambayo alisomewa mnamo siku ya Jumatatu.


Mbele ya hakimu mkazi wa Kwale Christine Njagi, mshukiwa huyo alikubali kuwa alikuwa akiishi na wanyama hao nyumbani kwake katika kijiji cha Mwamanga eneo la Msambweni bila ya kibali chochote kutoka kwa shirika la KWS.
Bi Njagi alitoa agizo hilo baada ya kobe hao pamoja na mamba mmoja ambaye pia anadaiwa kumilikiwa na mshukiwa huyo kushindwa kuwasilishwa mbele ya mahakama.


“Tumeweza kuwaona nyoka hao ambao tayari wameshapigwa picha ila hapo kesho (Jumanne) itabidi twende hadi nyumbani kwake ili tukawaone wanyama ambao wamesalia,” akasema Bi Njagi.


Kesi hiyo iliweza kuendelea baada ya nyoka hao kutolewa nje ya mahakama na kupigwa picha kama ushahidi hali ambayo iliwavutia watu wengi sana.


Kwa mujibu wa maelezo ya kiongozi wa mashtaka Eunice Gitau, mshukiwa huyo alipatikana na wanyama hao mnamo siku ya Jumamosi na maafisa wa KWS.


Hata hivyo Bi Gitau aliomba mahakama hiyo iupatie upande wa mashtaka mda wa wiki moja ili uweze kufanya uchunguzi wake kuhusu kesi hiyo.
Kusomewa upya mashtaka
“Upande wa mashtaka umeweza kushuhudia ushahidi wote ambao umewasilisha mbele ya mahakama hii ila tunaomba mda zaidi wa kufanya uchunguzi,” akasema Bi Gitau.


Hakimu huyo alikubaliana na ombi na kuisukuma mbele kesi hiyo hadi siku ya Jumatatu wiki ijayo ambapo mshukiwa huyo atasomewa upya mashtaka dhidi yake.


Vile vile alitaka ushahidi wote uweze kuwasilishwa katika mahakama hiyo wakati mshukiwa huyo atakapofikishwa mbele ya mahakama hiyo kwa mara ya pili.


Wakati huo wote Bw Galozi alikuwa amenyamaza kimya huku akiwa amejiwekea mikono yake mwili kifuani na kusubiri kufahamu hatima yake kuhusu kesi hiyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo