MTOTO WA MIAKA 9 AMUOKOA MAMA YAKE ASIUAWE NA MAMBA HUKO MPANDA

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri wa kipekee kwa kumwokoa mama yake mzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba baada ya kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.

Mama huyo mkazi wa kijiji cha Karema, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Mpanda, kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini Mpanda kwa matibabu baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto Ikola.

Akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea hospitalini hapo masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa miaka tisa aliyeweza kuokoa maisha yake licha ya kuwa amenyofolewa mkono na mamba huyo.

Akisimulia mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi akiwa anafua kando ya mto Ikola ghafla mnyama huyo aliibuka majini na kumpiga usoni na mkia wake.

“Mamba huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na mkia wake nami nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia mtoni ….binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona niko karibu kuliwa na mamba kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye … Alinishika mkono mwingine na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie hatimaye akaunyofoa mkono wangu na kutokomea nao mtoni ….” alieleza.

Aliongeza kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo wengi wao wakiwa wanawake walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na binti yangu walimvuta na kumtoa nje na baadae wakamkimbiza hospitalini mjini Mpanda kwa matibabu.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa amethibitisha kuwa hali ya mama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo