Jeshi la Polisi Ruvuma linasaka kundi la watu wanaodaiwa kuwa majambazi ambao walivamia na kuwapora pesa na mali zenye thamani ya Mil. 8 watu ambao walikuwa wakielekea msibani Songea vijijini.
Kamanda wa Polisi Ruvuma, Mihayo Miskhela amesema siku ya tukio Mei 7 kundi hilo la watu wakiwa na marungu na mapanga waliweka magogo na mawe barabani na kuliteka basi lililokuwa likisafirisha msiba huo na kuwapora vitu hivyo watu 22 waliokuwa wakisafirisha msiba.
Kamanda huyo amesema kuwa kundi hilo la watu tisa waliteka pia gari nyingine ikiwemo lori na gari ndogo pia na kuwapora vitu mbalimbali.
Watu hao waliwakamata na kuwapekua watu wote waliokuwa kwenye magari hayo huku wakiwa wamejifunga vitambaa vyeusi usoni na kisha kutokomea kusikojulikana.