JOTO la ubunge kwenye jimbo la Arusha Mjini, limezidi kupanda mara baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha, Francis Laizer kutangaza rasmi kuwania ubunge katika jimbo hilo, endapo akipewa ridhaa na chama chake kugombea.
Laizer amejitokeza kutangaza azma hiyo ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wa CCM, ambao ni Phillemon Mollel, Victor Njau,Thomas Munisi, Deo Mtui, Kim Fute kutangaza nia ya kuwania jimbo hilo linaloshikiliwa na mbunge wake, Godbless Lema(Chadema) ambaye tayari ametangaza kugombea tena.
Akizungumza na Mtandao huu jijini hapa, Laizer alisema amesukumwa na dhamira ya kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya kuwepo kwa changamoto nyingi, ambazo zimekosa mbunge wa kuzitatua kwa kipindi cha miaka mitano.
Alisema amefanya utafiti wa kina na kubaini changamoto lukuki zinazolikabili jiji la Arusha, ambazo zimeshindwa kutatuliwa na hivyo kuona ana uwezo mkubwa wa kufanya mabadiliko na kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Kada huyo alisisitiza kwamba miongoni mwa mambo ambayo atakwenda kuyafanyia kazi, pindi akifanikiwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo ni kushughulikia changamoto kubwa ya ajira kwa vijana na kinamama na wazee wa jimbo la Arusha Mjini.
Alitaja masuala mengine ambayo atatoa kipaumbele ni usalama wa raia na mali zao, kwani limekuwa ni tatizo kubwa kiasi cha kuharibu heshima na sifa ya jiji kwa matukio ya maandamano ya mara kwa mara yasiyokuwa na tija kwa maendeleo ya jiji.
Alisema kuwa Arusha ni mji wa kimataifa na kuwa umekuwa ukikabiliwa na changamoto ambazo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi wa kutosha, kwani matukio hayo yameharibu biashara ya utalii wa ndani na kupunguza ujio wa watalii kutoka nchi za kigeni na kupunguza mapato kwa jiji la Arusha na serikali kwa ujumla.
Hatahivyo, alibainisha kuwa atashughulikia changamoto nyingine ambazo zimedumu kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi zikiwemo za maji safi na salama, ujenzi wa shule za sekondari za kidato cha tano na sita kwa kata zote ili kuondokana na changamoto ya wanafunzi wanaofaulu kukaa majumbani kutokana na ukosefu wa madarasa