Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), amesema hana muda wa kulumbana na wanasiasa wanaotafuta ubunge kwa kutumia jina lake hasa kwa Ilala.
Amesema hatarudi nyuma kuwatumikia wapiga kura wake na sasa amejikita kuhakikisha anasimamia kutekelezaji Ilani ya Uchaguzi wa CCM na si kubishana na watu wanaotafuta ubunge kwa kutumia mitandao ya jamii ikiwamo facebook.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Zungu alisema kwa siku kadhaa watu watu wasioitakia mema Ilala wamekuwa wakitumia mitandao ya jamii kuchapisha vijarida kwa lengo la kumchafua mbele ya wapiga kura wake jambo ambalo amesema hawawezi kufanikiwa.
“Hizi fedha huwa zinatolewa kwa kigezo na hata matumizi yake huwa yanapangwa na kamati maalumu ambayo mbunge ni mwenyekiti tu na huwezi kuzikuta katika akaunti ya mbunge ila zinaingia katika halmashauri.
“…matumizi ni pamoja na kupanga matumizi ya miradi ya maendeleo lakini mwisho wa siku Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) huzikagua. Je, ni wapi Zungu anahusika, huu ni wakati wa uchaguzi Watanzania watarajie kuyaona mengi kutoka kwa wasaka tonge,” Zungu.
Alisema pamoja na hatua hiyo lakini hatayumba kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa wapiga kura wake.
Zungu aliwataka wanasiasa wanaomezea mate jimbo la Ilala wasiwe na hofu muda ukifika wakutane uwanjani kwa sababu waamuzi wa mwisho ni wapiga kura.