MWANAFUNZI wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kyela, iliyoko Mkoa wa Mbeya, Kharid Omary (13), amefariki dunia baada ya kupigwa na radi.
Pamoja kifo hicho, watoto wengine wawili walipoteza fahamu kutokana na radi hiyo.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni katika Kitongoji cha Bondeni, wakati mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali ilipokuwa ikinyesha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa wa Kitongoji cha Bondeni B, Kungaipe Nombo, alisema mtoto huyo alipigwa na radi alipokuwa mlangoni nyumbani kwao.
“Marehemu Omary na wenzake wawili ambao majina yao hatujayafahamu, walikuwa wanacheza na walipoona hali ya hewa inabadilika, waliagana na kurejea nyumbani kwao.
“Wakati Omary akiwa mlangoni nyumbani kwao, alipigwa na radi na kupoteza maisha,” alisema Nombo.
Naye baba wa marehemu ambaye pia ni Sheikh wa msikiti wa Al-Aqswa, Omary Juma, alisema wakati mwanae anapigwa radi hakuwa nyumbani.
“Wakati wa tukio sikuwa nyumbani na niliporudi, nilimkuta mwanangu akiwa amelala chini. Nilimchukua na kumkimbiza hospitalini, lakini sikufanikiwa kuokoa maisha yake kwa sababu tayari alikuwa ameshafariki,” alisema.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, Dk. Festo Dugange, alithibitisha kumpokea mtoto huyo na kusema wakati anafikishwa alikuwa ameshafariki.
