WANAWAKE wenye umri mkubwa wametakiwa kuacha kujihusisha na
mahusiano ya kimapenzi na vijana wenye umri mdogo, kwani jambo hilo
linawapunguzia heshima katika jamii.
Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima
Kihemba wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yaliyofanyika
eneo la Kituo cha Afya Mlandizi, wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Kihemba, ambaye kitaaluma ni mwanahabari, alisema kuna ripoti za
kipolisi mkoani Pwani zinazoeleza kuna kinamama ambao tayari
wamevuka umri wa miaka 60 wana uhusiano wa kingono na vijana
wenye umri mdogo, jambo linalowapunguzia heshima katika jamii.
“Kuna taarifa kuwa miongoni mwenu kuna kina mama wana tabia mbaya
ya kuwa na wapenzi ambao ni vijana wadogo sana kiumri.
Kweli si
kweli? Aliuliza mkuu huyo wa wilaya na wazee hao ambao kwa idadi
walikaribia 300, wakaitikia ‘Kweliiiii’.
Baadaye, Kihemba Alijibu juu ya ukubwa wa tatizo hilo mkoani humo ambapo alijibu; “Halijawa tatizo
kubwa sana, lakini kuna wachache walio na tabia hizo mbaya, ndio maana tunaanza kulidhibiti ili lisisambae kwa kasi maeneo
mengine.”
Alisema tatizo hilo kwa ukubwa lipo miongoni mwa wanaume ambao wamekuwa wakijihusisha na ndoa za utotoni kwa muda
mrefu, huku likilazimisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao kuolewa.
Uchunguzi uliofanywa miongoni mwa wazee ambao walikuwa wanapata huduma ya bure ya kupima afya zao kwa msaada wa
shirika lisilo la kiserikali la The Good Samaritan Social Services umethibitisha ubakaji na ndoa za utotoni ni matatizo makubwa
maeneo ya Mlandizi na viunga vyake.
Mkurugenzi wa Shirika hilo, Elisha Mwamkinga alisema shirika lake linajitahidi kuwaelimisha wazee kuishi kwa heshima katika
jamii na kuepuka mambo ya aibu miongoni mwao.
Kwa ufadhili wa Shirika la HelpAge International, zaidi ya wazee 300 wa Mlandizi walipima afya zao, na wengi wao wakapongeza
juhudi zinazofanya na shirika hilo katika kuwapa huduma mbalimbali za kiafya na chakula.