WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
kuna baadhi ya watu wamegeuza mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya
kuwa wa kisiasa badala ya kujikita kuwafahamisha wananchi mazuri
yaliyomo.
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa
wiki wakati akiwahutubia wakazi wa Kata ya Lwangwa kwenye Halmashauri ya
Busokelo wilayani Rungwe akiwa kwenye siku ya nne ya ziara yake mkoani
Mbeya kukagua shughuli za maendeleo. “Katiba inayopendekezwa
imezingatia maslahi ya kila kundi kwenye jamii hivyo zipuuzeni kauli
zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa Katiba hiyo haijakidhi malengo ya
Kitaifa,” alisema.
Alisema mabadiliko yaliyofanywa
kwenye Katiba hiyo ni asilimia 20, huku asilimia iliyobakia ni sehemu ya
mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba. Alisema ili
kukabiliana na kauli za kiupotoshaji, Serikali imeanza kusambaza nakala
za Katiba inayopendekezwa hasa kwenye mikoa ya pembezoni.
“Jumla ya nakala 300 za Katiba
Inayopendekezwa zitasambazwa kwenye kila Kata ambapo makundi yenye uwezo
wa kutoa elimu sahihi kuhusiana na Katiba inayopendekezwa yatapatiwa
nakala hizo ili kuwaelimisha wananchi,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huohuo, akiwa Tukuyu
mjini, Waziri Mkuu alizindua ofisi za Halmashauri hiyo baada ya jengo la
zamani kupata nyufa kutokana na tetemeko la ardhi. Pia alizindua
maabara tatu kwenye shule ya sekondari ya wasichana ya Kayuki.
Akizungumza na maelfu ya wakazi
waliojitokeza kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
uwanja wa michezo wa Tandale jana jioni, Waziri Mkuu aliwataka wakazi
hao kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha wakazi zoezi la uboreshaji
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litakapoanza.