Jeshi la polisi mkoani rukwa linawashikilia watu saba hadi sasa, kwa
tuhuma za kuhusika na kitendo cha kikatili cha kukata kiganja cha mkono
wa kulia, cha mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Baraka Cosmas Lusambo mwenye
umri wa miaka sita, katika kitongoji cha kikonde kata ya kipeta wilaya
ya sumbawanga vijijini, ambapo pia katika tukio hilo wamemjeruhi mtoto
huyo mkono wa kushoto.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa rukwa kamishna msaidizi wa
polisi Leons Rwegasira, amesema wamefanikiwa kuwakamata watu hao
kufuatia msako mkali, mara tu baada ya kutokea tukio hilo kwenye
kitongoji hicho cha kikonde, ambacho kinakuwa na wakazi wakati wa msimu
wa kilimo na kiangazi watu wanahama tena, katika familia yenye watoto
wengine watatu wenye ulemavu wa ngozi.
ACP.Rwegasira pia amesema kwenye msako huo mkali, wamefanikiwa
kuwakamata watu wanane wanaojihusisha na uganga wa jadi na upigaji wa
ramli chonganishi, ambacho ni chanzo kikubwa cha kusababisha vifo na
kujeruhiwa watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina.
Mtoto baraka na mama yake mzazi wamelazwa kwenye hospitali ya rufaa
ya jijini mbeya, wakitibiwa majeraha waliyoyapata wakati wa purukushani
za kumshambuliwa mtoto huyo.