SIKU mbili baada ya jeshi la polisi kuvamia nyumba moja katika Kata
ya Pasua katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, iliyotumika
kuhifadhi zaidi ya watoto 18 kinyume cha utaratibu, mmiliki wa nyumba
hiyo yenye vyumba vinne na choo kimoja, ameibuka na kujitetea licha ya
kwamba anashikiliwa na polisi.
Mmiliki huyo, Abdulnasir Abdulrahman amesema aliwakusanya watoto hao
wenye umri wa kati ya miaka miwili na 16 ili kuwafundisha masomo ya dini
ya Kiislamu na kuwakuza katika imani hiyo wakiwa wadogo.
Pamoja na utetezi huo, alisema watoto hao wameletwa hapo na wazazi
wao kupata elimu ya dini, na wazazi wao wanajua na wanachangia vitu
mbalimbali, ikiwemo vyakula ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya
dini ya kiislamu, “Watoto wote tunaoishi nao hapa wana wazazi wao,
ambapo wamekubaliana na sisi waaendelee kupata elimu hiyo hapa chini ya
uangalizi wetu na wazazi wao wamekubaliana niwalee,” alisema Abdulrahman
jana baada ya kukamatwa majira ya saa 5 asubuhi, tukio lililovutia
umati wa wakazi wa mji wa Moshi waliofurika katika nyumba hiyo na hata
Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Geofrey Kamwela alithibitisha
kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na pia baadhi ya wazazi wa watoto hao kwa
uchunguzi zaidi.
Katika nyumba waliyohifadhiwa watoto hao, polisi wenye silaha
walilazimika kutumia nguvu na mabomu kudhibiti umati wa wananchi
waliojitokeza kushuhudia kukamatwa kwa mmiliki na watoto.
Baada ya kufikishwa polisi, walirudishwa katika nyumba waliyokuwa
wamehifadhiwa wakiwa chini ya ulinzi, huku mmiliki na wazazi wakiendelea
kubaki polisi.
Jeshi la polisi linawashikilia baadhi ya wazazi na mmiliki wa nyumba
hiyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ambapo baada ya watuhumiwa hao
kukamatwa bado mamia ya wananchi hao waliongozana hadi kituo cha polisi.
Hadi gazeti hili linaenda mitamboni, bado wananchi walikuwa wamefurika nje ya geti hilo la kituo cha polisi.
Akizungumza na wananchi katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya
Moshi, Novatus Makunga alisema walipata taarifa kuwa eneo la Pasua, kuna
mtu mwenye kituo amehifadhi watoto kinyume na taratibu, na ndiyo kamati
ya ulinzi na usalama ilifika eneo la tukio na kukuta watoto hao katika
nyumba hiyo.
Alisema taarifa ya kuwepo kwa watoto hao waliipata wiki moja
iliyopita, lakini juzi Machi 7, mwaka huu, ndiyo jeshi la polisi
liliizingira nyumba hiyo kuanzia majira ya saa 12:05 jioni kutokana na
kukosa sehemu ya kuwahifadhi watoto hao Mkuu huyo wa wilaya alisema
kuwakusanya watoto sehemu moja bila kibali ni kinyume cha sheria, ambapo
mmiliki wa nyumba hiyo alipaswa kuomba kibali lakini pia mafunzo
anayoyatoa kwa watoto hao hata kama ni masuala ya dini ni lazima yafuate
taratibu za nchi.