Walimu wawili wa Shule ya Msingi Maalumu Mtindo na mwenyekiti wa
kamati ya shule hiyo wilayani Misungwi mkoani Mwanza, wamefikishwa
mahakamani kwa tuhuma za kuuza mafuta ya ngozi kwa ajili ya albino.
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru)
wilayani Misungwi, iliwapandisha kizimbani juzi kwenye Mahakama ya
Wilaya Misungwi washtakiwa hao kwa tuhuma ya makosa manne ya uhujumu
uchumi.
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Mwema Mella
aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Fredrick Mworo (42) ambaye ni Mwalimu
Mkuu Msaidizi na Mtunza Stoo, Velentina Ngodoki (34) mkazi wa Kijiji cha
Misasi ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Ngodoki Ginnery Supply,
Mwenyekiti wa kamati ya shule, Kalunde Kushamba (60) na aliyekuwa
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo mwaka 2012, Edesta Nshekanabo (32).
Mella alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja kati ya
Julai na Novemba 2012, walikula njama za kutenda kosa la kughushi mafuta
aina ya Neutrogena chupa 200 yaliyotolewa msaada na Hospitali ya Rufani
Bugando (BMC) kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (Albino) shuleni
hapo na kuyafanyia zabuni ya thamani ya Sh5.6 milioni.
Mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, wanadaiwa Julai
19, 2012 wakiwa shuleni hapo, walighushi muhtasari wa kikao cha kamati
ya shule kwa kuidhinisha ununuzi wa mafuta hayo, yaliyopokelewa ukiwa ni
msaada kwa albino.
Shitaka la pili na la tatu linawahusu mshtakiwa wa
kwanza na wa tatu wanaodaiwa kuwa Novemba 2, 2012, walitumia vibaya
nyaraka kwa lengo la kudanganya na kujipatia fedha, au faida kwa
kughushi hati bandia ya ununuzi namba 32/11 ya chupa 200 za mafuta aina
ya Neutrogena.
Shitaka la nne, tano na sita kwa washtakiwa wa
kwanza na wa tatu, wanadaiwa Novemba 11, 2012 walitumia nyaraka za uongo
za kudadisi bei kwa Kampuni bandia ya Madudi Ginnery Enterprises kwa
Sh6 milioni, huku kampuni nyingine bandia ya CJC Lab and Surgicals (T)
kwa Sh5.6 milioni.
Pia, mshtakiwa wa kwanza na wa pili wanadaiwa
Novemba 12, 2012, kwa kutumia nyaraka bandia kwa lengo la kudanganya na
kujipatia Sh5 milioni kwa kutumia hati ya malipo namba 11/15 kulipa
Kampuni ya Ngodoki kwamba wamepokea mafuta hayo.
Shtaka la nane kwa mshtakiwa wa kwanza, tatu na wa
nne, wanadaiwa kutumia vibaya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri
kwa kuitisha zabuni hewa ya Kampuni ya Ngodoki ya Misasi na kununua
chupa 200 za mafuta hayo ya ngozi kwa albino, yaliyotolewa bure na BMC.
Washtakiwa wote walikana mashtaka, wapo nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Mfawidhi, Godfrey Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 13, itakapoanza kusikilizwa.