Zaidi
ya migodi kumi na tano ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite
kitalu B kwenye machimbo ya Mererani wilayani Simanjiro imeteketea kwa
moto unaodaiwa kutokana na itirafu ya umeme na kusababisha hasara ya
zaidi ya shilingi bilioni nne na watu elfu mbili kukosa ajira.
Tovuti hii ilifika katika migodi hiyo na kushuhudia majengo mitambo ya
vifaa vingine vikiwa vimeteketea kwa moto na wasimamizi wa migodi hiyo
wakaeleza namna moto huo ulivyo anza huku wakidai kuwa ulilipuka wakati
wafanyakazi wa Tanesco walipokuwa wanafanya matengenezo ambao baada ya
moto kuwaka wamedaiwa kukimbia katika eneo ilo.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa kamati ya usuhuishi na
usalama wa migodi katika kitalu B Neene Lymo amesema hasara
waliyoipata ya zaidi ya shilingi bilioni nne ni kubwa hivyo wameitaka
serikali iwasaidie kwa kuwalipa fidia kwakuwa chanzo ni shirika la umma
huku wamiliki wa migodi hiyo wakidai kuna hujuma katika tukio ilo.
Mkaguzi wa migodi na baruti kutoka wizara ya nishati na madini
Henri Mditi amesema wataalam wa wizara wamefika na kuona eneo lililo
athirika lakini taarifa zaidi zitatolewa na kamishina wa madini kanda ya
kaskazini baada ya ukaguzi kukamilika.
Tovuti hii bado inafanya juhudi za kuutafuta uongozi wa shirika la Tanesco mkoa wa Manyara ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo.
Chanzo:ITV