SASA ni rasmi kwamba kazi ya kuliboresha Daftari la Kudumu la
Wapigakura nchini kote, itaanza Jumatatu ijayo Februari 16 na kumalizika
Aprili 29 mwaka huu.
Uandikishaji huo utaanzia katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara na Njombe na baadaye utahamia katika mikoa mingine.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema ratiba ya upigaji wa kura ya
maoni ambayo ni Aprili 30 iko pale pale, kama ilivyotangazwa na Rais
Jakaya Kikwete. Wakati uandikishaji huo ukianzia katika mikoa minne,
utafungwa kwa kumalizia Dar es Salaam na Zanzibar.
Akizungumza jana ofisini kwake, Mkuu wa Idara ya Elimu
ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Ruth Masham aliwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi katika uboreshaji wa daftari la wapigakura baada ya
utoaji wa elimu kwa waratibu kukamilika.
Alisema tume hiyo imetoa elimu kwa waratibu wa waandikishaji kwa kila
mkoa na katika kila mkoa wametoa mafunzo hayo kwa mratibu mmoja.
Pia, elimu imetolewa kwa maofisa waandikishaji wa Halmashauri, na
wasaidizi wao na hao ndio watakaotumika kutoa elimu kwa waandikishaji
wadogo katika ngazi za tarafa na kata.
Masham alisema ni haki ya kila Mtanzania kujiandikisha. Alisema
wananchi wana haki ya kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha ili ifikapo
Oktoba mwaka huu waweze kutumia haki hiyo ya kikatiba kuchagua viongozi
wanaowataka.
“Kila Mtanzania atapata fursa ya kujiandikisha na kupata kitambulisho
chake ambacho atakitumia wakati wa kupiga kura. Hivyo tunawaasa
watanzania wote wanaposikia uboreshaji umefika katika eneo lake
ajitokeze kujiandikisha,” alisema.
Katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda aliwahakikishia Watanzania kuwa uandikishwaji wa wapiga
kura ambao utatumia Mfumo wa Kielektroniki (BVR), utafanyika kwa ufanisi
na kwa wakati uliopangwa.
Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe kuhusu uhakika wa uandikishaji huo, Pinda alisema tume ya
uchaguzi inaamini kuwa vifaa vitakavyotumika, vina ubora mara mbili ya
vilivyoletwa kwa ajili ya uandikishaji wa majaribio.
Licha ya kukiri kuwa awali serikali ilikuwa na tatizo la kifedha,
Pinda alisema tume imewahakikishia kuwa shughuli zote za upigaji kura
kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, zitafanyika.
Pinda alimtoa wasiwasi Mbowe kuhusu ufanisi wa vifaa hivyo vya BVR,
kwa kusema endapo tume itaona kuwa uandikishaji huo hauwezekani kwa
sababu yoyote ile, itatoa taarifa bungeni na serikali iko tayari
kubadili maamuzi.