GWIJI wa muziki wa Bongo Flava, Rehema Chalamila, al-maarufu
Ray C amekanusha vikali uvumi ambao umekuwa ukisambaa Tanzania na Afrika
Mashariki kwa jumla kwamba amewahi kuwa na urafiki wa kimapenzi na Rais
Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Hata hivyo, Ray C, alikiri jinsi
alivyookolewa na Rais Kikwete kutoka katika janga la mihadarati baada ya
rais huyo kupata habari zake katika vyombo vya habari. Msanii huyo
ameanzisha kituo cha kuwafanyia marekebisho waathiriwa wa mihadarati
ambao wengi wao ni vijana.
Swali: Uliingiaje katika matumizi ya mihadarati?
JIBU: Mpenzi wangu wa zamani
aliniingiza katika janga hili. Sikujua mapema kwamba alikuwa mraibu wa
mihadarati nilipokutana naye kwanza. Wala sikujua tofauti ya bangi na
mihadarati mingine kutokana na ugeni wangu. Polepole nilijikuta
nikitumia dawa za kila aina. Mwili wangu ulianza kudhoofika huku
nikishindwa kukaa bila kutumia mihadarati. Mwili wote ungeniuma kama
ningekosa kutumia.
Swali: Unakumbuka ulitumia kiasi gani cha pesa kwa wiki katika hiyo mihadarati?
JIBU: Kilikuwa kiasi kikubwa mno
ambacho siwezi kukikumbuka. Machozi hunilengalenga kila ninapojaribu
kukumbuka. Wakati mmoja ilinibidi kuuza nyumba yangu, nikafunga maduka
na kuuza mali yangu nyingi ili nipate pesa za mihadarati. Nilijifunza
kwamba haijalishi kwamba u tajiri kiasi gani. Ukijiingiza katika
matumizi ya mihadarati lazima hatimaye ufilisike.
Swali:Je, familia yako ilijua kuwa ulikuwa umetumbukia katika janga la matumizi ya mihadarati?
JIBU: Nilijaribu sana kujificha
nikitaraji kuwa hali yangu haingetambulika. Hata hivyo, mamangu
alitambua mabadiliko niliyokuwa nayo. Sura yangu haikung’ara tena,
nikapoteza hamu ya kula na zaidi ya hayo nilikuwa mwepesi sana wa
kukasirika. Mama aliniita na kunishauri kuukata urafiki na mpenzi wangu
ambaye alimjua kama mzoefu wa kutumia mihadarati lakini nikapuuza
ushauri huo.
Swali: Uliamua lini kuacha matumizi ya mihadarati?
JIBU: Ulikuwa mwaka 2012 ambapo
niliamua ama nijiue au niende jela. Nilikuwa nimechoshwa na utumwa wa
mihadarati. Sikuona maana ya maisha ikiwa kila senti niliyoipata
iliingia katika mihadarati. Niliachana na mpenzi wangu. Kama mamangu
hangekuwepo kunishughulikia sasa hivi stori ingekuwa tofauti.
Swali: Je, uliweza kuacha matumizi hayo ya mihadarati tu ghafla kama umepunguza tu kama watu wasemavyo?
JIBU: Wajua watu wanayo mengi sana
ya kusema na huwezi kuwazuia. Rais Kikwete alipojitolea na kunisaidia
nilijikaza kisabuni na kuachana na mihadarati. Nilitaka kuachana na aibu
yangu ya kutajwatajwa hadharani kama mwathirika wa matumizi ya
mihadarati na Mola ameniwezesha kufikia lengo langu.
Swali: Je, Rais Kikwete alijuaje shida yako na kunao ukweli wowote kwa mlikuwa na urafiki wa kimapenzi?
JIBU: Sina hakika sana ila nakisia
tu kwamba ilikuwa kupitia katika vyombo vya habari hasa magazeti na
radio baada ya mamangu kuzungumza na waandishi wa habari. Kuhusu urafiki
hilo nakanusha kabisa kwa maana ilikuwa mara yangu ya kwanza kumwona
akiwa karibu nami na ninamshukuru sana kwa ukarimu wake ambao umeniweka
hai hadi leo. Nitamwombea Mungu ambariki katika kila alifanyalo.
Swali: Je, kumekuwa na mabadiliko yoyote kwako tangu uache mihadarati?
JIBU: Sasa ninaishi maisha ya
uhakika. Najisikia kuwa mwenye afya. Lakini sina imani tena na wanaume
na nitakaa kwa muda bila kuwa na urafiki nao na ikiwa ni lazima urafiki
huo uwepo basi nitamtafuta mwanamume wa miaka 60 na zaidi. Sitataka
urafiki na vijana tena kwani huo ndio ulioniingiza katika mateso
niliyopitia.
Swali: Umekaa miaka kadhaa bila kuwa katika ulingo wa muziki. Huoni kuwa umesahaulika?
JIBU: Umahiri wangu nauona uko pale
pale. Ni kweli kuna mabadiliko makubwa na mazuri katika muziki chapa
Bongo Flava. Hata hivyo, kwa vigogo kama sisi tunasalia pale pale;
tunaona wageni wakija na kupita kama moshi tu huku sisi tukisalia pale
pale tukiendelea kuimarika tu. Tayari nimetayarisha albamu mpya na
nasubiri wakati mwafaka kuizindua.
Swali: Umefungua kituo cha
Ray C Foundation kusaidia walioathiriwa na mihadarati. Je, unatarajia
kumsaidia mpenzi wako wa zamani pia?
JIBU: Ni hiari yake. Siwezi
kumlazimisha. Ni vigumu sana kumlazimisha mtu kubadilisha mwenendo wake.
Hata hivyo, akija nitakuwa tayari kumpokea na kumsaidia.
Swali: Je, ni kweli wanavyodai mashabiki wako kuwa umeichubua ngozi yako ili uonekane mweupe zaidi?
JIBU: Hata kidogo na wala
sidhamirii kufanya hivyo karibuni. Kunawiri kwa ngozi yangu kwatokana na
afya nzuri ambayo imeanza kurudi hivi karibuni.
Swali: Tumekaa sana bila kitu kipya kutoka kwako. Unatupa nini hivi karibuni?
Jibu: Tayari nimerekodi albamu mpya
ingawa meneja wangu anasisitiza tusubiri hadi wakati mwafaka uwadie
ndipo tuachilie ngoma hizo. Nina hakika mtazifurahia.