Jeshi la Polisi Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, limeingia katika kashfa baada ya askari wake kutuhumiwa kumuua raia.
Raia
huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mdonga, fundi wa magari, Januari Mtitu
(20), inadaiwa kuwa aliuawa kwa risasi na askari mwenye namba G 6352,
Abduel Nyuki.
Tukio hilo lilitokea Januari 23, mwaka huu, saa 7:00 usiku, na mtuhumiwa anafanya kazi katika Kituo cha Polisi Ludewa.
Mkuu
wa Wilaya ya Ludewa, Juma Madaha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kuwa tayari askari anayetuhumiwa na raia wengine wawili, wamekamatwa.
Habari
zinaeleza kuwa wakazi wa eneo la tukio, walipandwa na hasira na
kumfanya Mkuu wa huyo wa Wilaya kulazimika kuwatuliza kwa kuwataka
wapunguze hasira ili wasiwadhuru polisi wengine kwa sababu siyo wote
waliohusika na tukio hilo.
Kauli
ya Mkuu huyo wa Wilaya ilitokana na mgomo wa mafundi wa magari kukataa
kutengeneza jeneza na kutaka kuandamana huku wakilitaka Jeshi la Polisi
kulitengeneza wenyewe ama kulipa fedha kwanza ndipo litengenezwe.
“Sasa
hivi tumechoka kuteswa na kunyanyaswa na polisi, wanaacha kukamata
wahalifu badala yake wamewageukia wananchi ambao hawana hatia na leo hii
wamemuua mwenzetu bila kosa,” mmoja wa mafundi hao alisema.
Mdogo
wa marehemu, Imani Mtitu, alisema kabla ya kupigwa risasi, kaka yake
alisikia akizungumza na mtu kwa njia ya simu huku wakijibizana kwa ukali
na baada ya muda mfupi, walifika watu wakagonga mlango wa marehemu na
alipokataa kufungua, waliuvunja na muda mfupi ulisikika mlio wa bunduki.
“Nilipotaka
kutoka ili kumpa msaada kaka yangu, niligundua kuwa mlango umefungwa
kwa nje na nilipofanikiwa kutoka nilikuta marehemu (Mtitu) akiwa amelala
chini damu zinatoka, lakini anashindwa kuongea,” alisema Imani.
Mkuu
wa Polisi Wilaya ya Ludewa, Galiya Moshi, alisema chanzo cha tukio hilo
ni askari Nyuki akiwa lindoni kwake katika Benki ya NMB tawi la Ludewa,
alipigiwa simu na mpangaji mwenzake kwamba katika chumba chake kulikuwa
na wizi, ndipo alipoacha lindo saa 7:00 usiku na kumfuata marehemu
nyumbani kwake baada ya kutajwa na rafiki zake kuwa ndiye aliyehusika.
Moshi alisema kuwa watu wengine wawili ambao majina yao tunayahifadhi, wanashikiliwa na polisi.
Watu hao wanashikiliwa kutokana na kumpeleka askari huyo nyumbani kwa marehemu.
Alisema
kuwa katika upekuzi, marehemu alikutwa na vielelezo mfukoni mwake
ambavyo ni ‘flash’ na ‘remote’ ya tv, vitu ambavyo vilitambuliwa na
mtuhumiwa.
Licha
ya kuwa na mvutano huo, marehemu alizikwa katika makaburi ya Lugarawa
mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya baada ya mvutano mkali
uliokuwapo kati ya wananchi wa kijiji cha Lugarawa, wazazi na Polisi
ambao walikuwa wakituhumiwa kumuua marehemu kwa makusudi.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kueleza kuwa askari huyo ameshafukuzwa kazi.