LEO Tanzania inaanza kutekeleza hatua muhimu ya kutimiza matukio
mazito, yanayosubiriwa kwa hamu mwaka huu na Watanzania nchi nzima ya
upigaji kura ya maoni katika Katiba Pendekezwa na uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Hatua hiyo muhimu ni kuanza rasmi kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la Wapigakura kupitia mfumo mpya wa Biometric Voters Registration
(BVR), ambao unaanza leo mkoani Njombe.
Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilishaufanyia majaribio mfumo
huo katika baadhi ya maeneo ndani ya mikoa mitatu ya Dar es Salaam,
Morogoro na mkoani Katavi.
Kwa mujibu wa taarifa ya tume, pamoja na changamoto chache
zilizobainika, katika maeneo hayo tume ilifanikiwa kwa asilimia kubwa na
ina uhakika mfumo huo utatumika kuwaandikisha Watanzania wote katika
daftari hilo bila matatizo.
Tume hiyo ilitaja changamoto chache zilizojitokeza katika majaribio
hayo kuwa ni mfumo mzima wa BVR ulivyoandaliwa (setting), hardware na
programu zinazotumiwa na mfumo huo na maeneo ya uendeshaji uandikishaji
huo.
Tume hiyo imewahakikishia Watanzania kuwa changamoto zote hizo,
zimefanyiwa kazi kwa kurekebishwa, ambapo pia BVR zitakazotumika mkoani
Njombe, nazo zimefanyiwa marekebisho kutokana na changamoto
zilizojitokeza.
Kutokana na maandalizi hayo ni wazi kuwa sasa utaratibu mzima wa watu
kujiandikisha katika daftari la kudumu, unaanza rasmi mkoani Njombe.
Hivyo, ni vyema wakazi hao wakajitokeza kwa wingi na kutumia haki yao
ya kujiandikisha ili waweze kushiriki vyema katika matukio mawili
makubwa ya uchaguzi.
Hapa nchini katika chaguzi nyingi zilizopita, ilizoeleka kuona idadi
ndogo ya watu wenye umri wa kupiga kura kujitokeza kupiga kura, jambo
linalosababisha hata ushiriki katika uchaguzi na wale wanaojitokeza
kupiga kura pia uwe mdogo.
Ikumbukwe kuwa kila mtu aliyetimiza miaka 18 ana haki ya
kujiandikisha katika daftari hilo na kushiriki kikamilifu katika
uchaguzi wa kura ya maoni kupigia kura Katiba Pendekezwa na pia
kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kuchagua viongozi
watakaoliongoza taifa.
Hivyo basi ni vyema wakazi wa Njombe, wakawa mfano mzuri kwa
watanzania wa mikoa mingine inayosubiri utaratibu huo wa kujiandikisha,
kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili ratiba ya uandikishaji
itakavyosogea katika mikoa mingine, watu wawe na mwamko wa kushiriki
kikamilifu.
Wapo baadhi ya watu kazi yao ni kulalamika, kunyoosha vidole na kuishia kufanya vurugu matukio muhimu kama hayo yanapojitokeza.
Watu kama hao badala ya kujitokeza na kushiriki, hutafuta visingizio
na baadaye wanapokosa fursa ya kushiriki katika uchaguzi huwa wa kwanza
kuanzisha vurugu. Tutambue kuwa kila Mtanzania ana haki ya kupiga kura
pale atakapofikisha umri wa miaka 18.
Ikumbukwe pia kuwa mtu hawezi kushiriki katika uchaguzi huo na
kumchagua kiongozi anayemtaka, kama hatajiandikisha katika daftari hilo
la wapiga kura.
Hivyo basi, wakazi wa Njombe watambue kuwa macho na masikio ya
watanzania wote kuanzia leo yapo mkoani humo, wakifuatilia kwa kina
utaratibu mzima wa kujiandikisha katika daftari hilo, hasa kupitia mfumo
huo wa BVR, ambao umezua gumzo nchini tangu utambulishwe na NEC.
Kutokana na ukweli huo, ni wajibu kwa wakazi wa Njombe kushiriki kikamilifu katika shughuli hiyo.
Pia, tume yenyewe ni lazima ihakikishe kuwa ahadi iliyotoa kwa
watanzania, kupitia matokeo ya majaribio ya uandikishaji wananchi
kupitia mfumo huo wa BVR, inatekelezeka na uandikishaji huo mkoani
Njombe unafanyika kwa mafanikio.