JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limewataka vijana waliomaliza katika
jeshi hilo, kutambua kuwa walikula kiapo cha utii wakati wa kuhitimu
mafunzo, hivyo suala la kuandamana ni kinyume na kiapo chao.
Vijana hao waliotumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na
kumaliza mkataba wa miaka miwili, wameambiwa shinikizo lao la
kulazimisha ajira kwa kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makao Makuu ya jeshi
hilo, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, ilisema kipengele kimoja
cha masharti ya kujiunga na JKT kinasema baada ya mkataba, wanapaswa
kurejea nyumbani na hawapaswi kudai jeshi liwatafutie ajira. Ilieleza
kwamba masharti ya jeshi hilo, huwekwa bayana kwa vijana wanapojiunga na
JKT.
Vijana hao wanatakiwa kujua masharti hayo na taratibu za JKT na
kuelewa kuwa JKT halitoi ajira. Taarifa hiyo ilinukuu kipengele
kimojawapo cha masharti, kinachosema “Kwa kipindi chote nitakachokuwa
ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya mafunzo ya kijeshi na
ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea nyumbani.
Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie
ajira/ kazi”.
Ufafanuzi huo ulitolewa, kutokana na vijana zaidi ya 200 waliohitimu
mafunzo ya JKT kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2013, kutangaza wiki
iliyopita kuwa wataandamana siku yoyote wiki hii kwenda kwa Rais Jakaya
Kikwete, kumweleza shida zao, ikiwemo kutokuwa na ajira tangu wamalize
mafunzo.
Jeshi hilo lilisema ni vema vijana hao, wakatambua kuwa tatizo la
ajira siyo kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania, ikiwemo
hivyo wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.
“Kutokana na dhumuni la kuundwa JKT Taifa, halina dhamana ya kuajiri
bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo baada
ya hapo wawe wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi
mbalimbali za serikali na binafsi,” ilisema taarifa hiyo.
Hata hivyo, jeshi hilo limesema tangu mwaka 2003 hadi 2014, vijana
24,708 wameajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya hao,
vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670, wameajiriwa
na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Kwa upande wa Polisi, vijana 3,965 wameajiriwa ambao kati yao,
wavulana ni 2,943, Magereza wameajiriwa 2,139 kati yao wavulana ni
2,044, Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa 78 na taasisi zingine
wameajiriwa vijana 592.
Aidha, vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama vile
migodi ya dhahabu ya Geita, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Shirika
la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Taarifa hiyo ilisema JKT ilianzishwa Julai 10, 1963 kwa lengo la
kuwaweka pamoja vijana na kuwapa malezi, kuhusu uzalendo na umoja ili
kuondoa dalili za matabaka, zilizoanza kujitokeza katika jamii baada ya
uhuru.
Serikali ilirejesha mafunzo ya jeshi hilo kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001 baada ya kusitishwa mwaka 1994.