MAMA wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yojana Bahati (1), Ester
Thomas aliyelazwa katika hospitali ya Bugando akipatiwa matibabu baada
ya kujeruhiwa, ameelezea jinsi alivyovamiwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na mwandishi wetu, Ester (30) alisema
alijeruhiwa juzi nyakati za usiku na watu wasiojulikana mkoani Geita
baada ya kumvamia nyumbani kwao na kumpora mtoto wake mwenye ulemavu wa
ngozi.
Akizungumza kwa shida hospitalini hapo, Ester alisema alivamiwa akiwa
amelala na mtoto wake huyo ambapo walimkatakata kwa mapanga sehemu
mbalimbali za mwili na kisha kutokomea kusikojulikana.
Naye Mkuu wa kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dk Derick David
alisema mgonjwa huyo alipokewa juzi saa nane mchana akitokea mkoani
Geita.
Daktari alisema mgonjwa huyo ambaye hali yake sio ya kuridhisha,
alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kutokana na kukatwa panga kwenye
paji la uso pamoja na kukata sehemu ya mfupa wa pua.
“Tunamshukuru Mungu mgonjwa huyu anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa
upasuaji kwani kwa sasa hali yake ni tofauti na alivyopokewa,” alisema.
Alisema mama huyo anaendelea na matibabu ya majeraha na pia atapatiwa
na huduma ya kisaikolojia kutokana na maumivu makali aliyonayo ya
kuporwa kwa mtoto wake.