Baraza la maadili ya utumishi wa umma limeshindwa kumuhoji mbunge wa
Bariadi Magharibi Mh Endrew Chenge baada kuwasilisha zuio la mahakama
kuu lililozua kutokuendelea kujadili miamala ya Escrow huku wanasheria
wa sekretarieti ya baraza hilo wakipingana naye kwa madai kuwa wao
wanajadili ukiukwaji wa maadili na siyo miamala ya Escrow.
Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi
Msumi ameahirisha kikao hicho hadi Feb 26 mwaka huu ili wajumbe wapate
muda wa kupitia zuio hilo ambapo baraza litakuja na uamuzi ama wa
kuendelea au kusitisha hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wa sakata
hilo.
Akisoma hati ya malalamiko dhidi ya Chenge, mwanasheria wa
sekretarieti ya maadili, Hassan Mayunga amesema mlalamikiwa amekiuka
maadili ya viongozi wa umma ambapo akiwa mwanasheria mkuu wa serikali AG
mwaka 1995 aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na kampuni
ya Independent Power Solution Limited IPTL wa kuongeza uzalishaji wa
umme.
Aidha ameongeza kuwa wakati anafanya hayo hakuweka wazi kuwa ana
maslahi binafsi na baada ya kustaafu wadhifa huo Desemba 2005 aliingia
mkataba wa kuwa mshauri mwelekei wa kampuni ya Vip Engineering and
Marketing Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL
kitendo ambacho ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma
ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha na utumishi wake
uliopita.
Akitetea hoja yake ya kutaka baraza hilo lisitishe zoezi la
kumuhoji Mh Chenge amesema malalamiko dhidi yake ni chimbuko la uamuzi
wa bunge na kutaka apewe mwongozo wa suala hilo kuendelea kujadiliwa
wakati mahakama kuu imeshazuia huku akilitaka baraza hilo kutokuingia
kwenye misukumu ya kisiasa badala yake wafuate sheria za nchi na
kukabidhi hati hiyo kwa mwenyekiti wa baraza.
Hata hivyo mara baada ya kutoka nje ya ukumbi waandishi kutoka
vyombo mbalimbali vya habari walipotaka kufanya naye mahojiano juu ya
suala hilo Mh Chenge majibu yake yalikuwa hivi.
Mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi Msumi akizungumza
mara baada ya kuahirisha zoezi hilo amesema amelazimika kufanya hivyo
ili wapate fursa ya kupitia zuio hilo ili kila upande uweze kupata haki.
Kwa upande wa wanasheria wa sekretarieti ya baraza hilo wamepinga
hoja alizotoa mh Chenge na kudai kuwa wao walipitia zuio hilo na kufanya
uchunguzi wa kina kabla ya kumuta na awali walishafanya naye mahojiano
lakini hakutoa hoja hizo.