WATU wanaojihusisha na mauaji ya albino kwa lengo la kusaka vyeo au
utajiri, wameonywa waache tabia hiyo mara moja kwa kuwa Mungu anawaona
na kuchukizwa na vitendo vyao.
Aidha, wametakiwa kutambua kuwa vitendo wanavyovifanya si tu
vinaukwaza utawala wa duniani na kuleta maumivu kwa wanajamii, bali
vinawafanya wajifungie milango ya mbinguni, kwa sababu, inafunguliwa kwa
wenye matendo mema pekee na si wauaji.
Hayo yalisemwa na Askofu wa jimbo la Rulenge, Mhashamu Severin
Niwemugizi wakati wa mahubiri kwenye ibada ya maziko ya aliyekuwa Askofu
mstaafu wa Kanisa Katoliki, jimbo la Tunduru-Masasi, Mhashamu Askofu
Magnus Mwalunyungu (85) aliyefariki hivi karibuni.
Askofu Niwemugizi, amesema kukatisha maisha ya mwingine, au kumtia
kilema mtu mwingine ni dhambi ambayo binadamu anaweza kukwepa adhabu
yake hapa duniani tu kwa kujificha asionekane, lakini akakamatwa na
Mwenyezi Mungu na kuhukumiwa kwenye moto wa milele, siku ya hukumu yake
itakapofika.
Askofu Niwemugizi alisema, njia zote hizo ovu zinazotumiwa na
wanadamu kupanda kifedha na utawala zitaendelea kuwa mbwembwe tu za
duniani, lakini mafanikio ya kweli na halali yatatokana na watu kujituma
kufanya kazi kwa bidii, huku wakilindana na kusaidiana kwa upendo.
“Unamfanyia binadamu mwenzako ukatili na kuamini kuwa huonekani
machoni pa watu, unamkata na kuondoa viungo vya mtoto mdogo mwenye
ulemavu wa ngozi na kuvitumia kwa mambo yako ya kujiinua, kwa sababu
mtoto huyo hawezi kujipigania na kukushitaki, ewe mwanadamu, acha
kufanya hivyo kwa kuwa Mungu anakuona”.
“…Kila anayefanya ukatili huo atambue kuwa anaukana ufalme wa
mbinguni. Ninafahamu kuwa wanaofanya hivyo ni wanajamii wenzetu wenye
dini, walio batizwa kama ni wakristo, na wenye akili timamu zinazotosha
kuwafanya watambue jema na baya.
Ni watu wenye makusudi na roho mbaya, ambao humkana Mungu na kutafuta
kujikweza kwa njia hizo zisizofaa,” Askofu Niwemugizi alisema.